03 January 2013

SUMATRA- Operesheni kamata daladala imefanikiwa



Na Grace Ndossa

MAMLAKA ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu(SUMATRA) imesema kuwa oparesheni iliyoendeshwa ya kukamata daladala korofi zilizokuwa zinakatisha ruti zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa baada ya madereva wengi kutii sheria za barabarani .


Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Mfawidhi kanda ya Mashariki Bw. Konrad Shio alipokuwa anazungumza na gazeti hili kuhusu oparesheni ya kukamata daladala korofi,kukatisha ruti pamoja na kupandisha nauli nyakati za jioni.

Alisema kuwa oparesheni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na daladala zilizokuwa korofi na kukatisha ruti kufuata sheria na kanuni za barabarani.

"Oparesheni ya kukamata daladala korofi  zinazokatisha ruti na kupandisha nauli jioni  iliyoanza Novemba mwaka huu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madereva wengi kuogopa kufungiwa pamoja na kulipa faini,"alisema Bw.Shio.

Pia alisema kuwa oparesheni hiyo ni endelevu hadi kila dereva aweze kutii sheria za barabarani na kuacha tabia ya kukatisha ruti na kutoza nauli kiwango kilichopangwa.

Bw. Shio alisema kuwa oparesheni hiyo iliweza kufungia daladala 40 kwa muda wa mwezi mmoja na  nyingine  365 kutozwa faini ya sh. 250,000.

Hata hivyo alisema kuwa  kwa sasa wanashirikiana na Baraza la usalama barabarani katika oparesheni  katika kituo kikuu cha mabasi ubungo  kukagua mabasi ambayo ni mabovu na yale yanayopandisha nauli.

Alisema kuwa oparesheni hiyo inafanyika mikoa yote na itakuwa endelevu hadi waweze kuondoa mabasi yote mabovu

No comments:

Post a Comment