07 January 2013
Serikali yatoa msaada wahanga wa mafuriko Igunga
Moses Mabula,Igunga
WAHANGA wa mafuriko ya mvua katika wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamepatiwa msaada wa vitu mbali
mbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma
Mwassa,Mkuu wa Wilaya ya Igunga,Elibariki Kingu, alisema kuwa Serikali imetoa mahema 50,mikeka 242, blanketi za watoto 100 na blanketi za wakubwa 242.
Mkuu huyo wa wilaya amevitaja vitu vingine
vilivyotolewa na serikali ni kwa ajili ya kuzisaidia kaya 62 zilizoathiriwa na mafuriko ni mikoba ya dawa 100 kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya mlipuko na maboksi 100 ya vifaa mbalimbali vya usafi.
Alisema pamoja na vifaa hivyo serikali pia imetoa
tani 12 za mahindi kwa ajili ya kuwasaidia wahanga hao na kutoa vyandarua 242 ili kuwanusuru na ugonjwa wa malaria.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Igunga, amemweleza mkuu wa
mkoa kwamba serikali imetoa pia kiasi cha sh. 612,000 kwa ajili ya kusafirishia mahindi hayo kutoka katika ghala la chakula mkoani Shinyanga hadi
Igunga mkoani Tabora kazi ambayo alisema imekwisha kamilika.
Alisema msaada huo wa serikali umetolewa na ofisi
ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa umetokana na athari zilizosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha wiki mbili zilizopita ambazo zilisababisha kaya 62 katika vijiji vya Mayunge na Igunga Mashariki nyumba zao kuanguka.
Alisema maafa hayo yamewaacha watu 242 wakiwa
hawana makazi na kwamba serikali wilayani humo imewahifadhi katika majengo ya Serikali kama zahanati shule na kadhalika.
Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Tabora Bi.Mwassa
aliwapa pole wananchi hao kwa niaba ya serikali na ofisi ya waziri mkuu kwa maafa waliyoyapata kutokana na janga la mvua za masika na kuwataka wawe
wavumiliavu wakati serikali ikiendelea na jitiada za kuhakikisha wananchi wanapatiwa sehemu zingine za kuishi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment