14 January 2013

Polisi 5 mbaroni upotevu mil.150/- *Ni zile zilizoporwa na majambazi Kariakoo *Kova akaribisha wananchi kutoa ushahidi


Darlin Said na Leah Daudi

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia askari wake watano kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa fedha sh. milioni 150, zilizoporwa na majambazi katika eneo la Kariakoo, Mtaa wa Mahiwa na Livingstone, mwaka 2012.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchunguzi uliofanywa na jopo la upepelezi kutokana na madai ya baadhi ya polisi kuhusika na wizi wa fedha hizo.

Alisema katika uchunguzi huo, wamebaini polisi watano walihusika na upotevu wa fedha hizo kwa namna moja au nyingine hivyo hatua waliyochukua ni kuwakamata na kuwahoji.

“Askari hawa walihojiwa ili haki iweze kutendeka, tunawaomba watu wengine waliokuwepo katika eneo la tukio, wajitokeze ili waweze kutoa ushahidi kwa maana ya kuwatambua,” alisema.

Kamanda Kova aliongeza kuwa, uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika, jeshi hilo litachukua hatua ya kuwashughulikia polisi hao kijeshi na jarada la kesi hiyo litapelekwa kwa wakili
wa Serikali kwa upepelezi zaidi ili kujiridhisha zaidi na kama
wana hati watafikishwa mahakamani.

Alisema mbali ya jeshi hilo kuwashikilia polisi hao, pia wanawashikilia majambazi wawili ambao walihusika katika tukio hilo Bw. Deogratias Kimaro (30) na Bw. Kulwa Mwakabala (30), ambapo wote wapo mahabusu.

Wakati huo huo, Kamanda Kova amewataka wananchi kuwa na imani na jeshi hilo ambalo linafanya kazi kwa kuzingatia maadili
na haki ya kila mtu bila kujali cheo chake.

“Ile dhana ya Jeshi la Polisi haliwezi kuchunguza askari wake wanpofanya makosa haina ukweli wowote, hata kiongozi wa
juu wa jeshi akikiuka maadili, sheria itafata mkondo,” alisema.

Alisema mwaka 2012, jeshi hilo limewafukuza kazi askari 20 wa kanda hiyo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya utoro kazini na kushtakiwa kijeshi zaidi ya mara moja.

Desemba 14,2012, Kampuni ya Altan Ltd inayouza matairi eneo la Kariakoo, lilivamiwa na majambazi watatu waliokuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili T 301 CCW, ambao walipora sh. milioni 150 na kusababisha vifo vya watu wawili.

Siku chache baada ya tukio hilo, watuhumiwa wawili Bw. Augustino Kayula na Bw. Frank John Mwangimba, walikamatwa wakiwa na bastola aina ya Browning lakini hawakuwa na fedha zilizoporwa.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa, fedha hizo ziliporwa na baadhi ya polisi waliokuwa eneo la tukio hivyo kutokana na taarifa hizo, waliamua kuunda jopo la wapelelezi ili kufanya uchunguzi wa kina.

Katika hatua nyingine, Kamanda Kova amekanusha taarifa ambazo zilitolewa katika vyombo vya habari kuwa, jeshi hilo liliunda tume ya kuchunguza watu walihusika kumteka Dkt. Steven Ulimboka.

“Naomba kuweka sawa jambo hili, sisi tuliunda jopo la wapelelezi kuchunguza tukio la kutekwa Dkt. Ulimboka si tume kama ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari,” alisema.

Alisema taarifa hizo zimemsababishia usumbufu mkubwa akitakiwa kutoa ufafanuzi wa tume hiyo imefikia wapi katika uchunguzi wake.

No comments:

Post a Comment