07 January 2013

Manispaa Songea yapandisha kiwango cha ushuru


Na Stevan Augustino,Songea

MANISPAA ya Songea Mkoani Ruvuma imepandisha kiwango cha kutoza ushuru kwa wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao ndani ya masoko yote yaliyopo katika manispaa ya hiyo.


Taarifa za ongezeko la ushuru huo zinaeleza kuwa  zoezi hilo limefanyika baada ya kukamilika kwa zoezi kubwa la kuwahamisha kwa kasi wafanyabiashara waliokuwa wakiendesha shughuli zao za kibiashara katika maeneo yasiyo rasmi .

Akifafanua taarifa hiyo Mkuu wa Masoko ya Manispaa ya Songea Bw.Salum Homera alisema kuwa ushuru huo umeongezwa kwa asilimia 100 kutoka sh.200 mpaka 400 kwa kila mfanyabiashara kwa siku.

Bw.Homera aliendelea kufafanua kuwa ongezeko hilo ambalo tayari limeridhiwa na wafanyabiashara limeanza kutekelezwa tangu Januari Mosi,mwaka huu ingawa lilitangazwa na uongozi wa halmashauri ya manispaa hiyo tangu Julai mwaka 2011 lakini wafanyabiashara walipinga wakishikiza kuondolewa kwa wafanyabiashara waliokuwa nje ya masoko ambao walikuwa hawalipi ushuru.

Alisema baada ya pingamizi hilo la wafanyabiashara waliokuwa ndani ya masoko halmashauri ililazimika kuendesha operesheni maalumu ya kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwa wakiendesha biashara zao kiholela ikiwemo kandokando mwa barabara.

Aidha mkuu huyo wa maasoko aliwataka wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa kulipa ushuru huo pamoja na ongezeko hilo ili kuiwezesha halmashauri kutekeleza majukumu muhimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwapatia fursa na mahitaji yao muhimu.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyabiashara walisema kuwa wameridhishwa na hatua zilizochukuliwa za kuwaondoa wafanyabiashara wa nje ya masoko na kuwahimiza kuingia ndani ya masoko ili nao waweze kulipa ushuru na kuomba zoezi hilo la kuwaondoa wafanyabiashara holela liwe la kudumu.

No comments:

Post a Comment