21 January 2013

Bulembo atishia ajira za watendajiPeter Mwenda na Andrew Ignas

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Abdallah Bulembo, ametishia kuwafukuzisha kazi watendaji wa Serikali ambao watabainika kutoa ushirikiano kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).


Miongoni mwa watumishi wanaokabiliwa na tishi hilo ni pamoja na Wakurugenzi, madaktari, wahandisi, Maofisa Watendaji wa kata na mitaa.

Bw. Bulembo aliyasema hayo juzi katika siku ya kwanza ya ziara yake jijini Dar es Salaam wilayani Temeke na kuongeza kuwa, baadhi ya watendaji Serikali wana tabia ya kutoa ushirikiano
kwa viongozi wa CHADEMA.

Aliwataka Watanzania, kuachana na CHADEMA na kudai chama hicho kinatawaliwa kwa matakwa ya Mwenyekiti wake, Bw. Freeman Mbowe.

“CCM ndio chama pekee chenye sera za kuwakomboa Watanzania, msidanganyike na CHADEMA, ambacho kina malengo binafsi ya
kutaka kujinufaisha na rasilimali za nchi ndio maana hata wenyewe
wanasema chama chao cha kifamilia,” alisema Bw. Bulembo.

Alisema CCM haiwezi kufumbia macho suala la rushwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya kwenye hospitali zilizojengwa kwa sera ya chama ili kuboresha maisha ya wananchi.

“Nitahakikisha mwaka 2015, jumuiya inapata nafasi za uwakilishi wa Viti Maalumu bungeni, sisi hatuna tofauti na jumuiya nyingine,” alisisitiza na kuongeza kuwa, jumuiya hiyo ina rasilimali nyingi ikiwa na shule za sekondari 70, lakini bado wanashindwa kufikia malengo waliyojiwekea.

Katika hatua nyingine, Bw. Bulembo aliwapongeza wanachama wapya 850 kwa kuchukua uamuzi wa kuhamia CCM wakitokea
vyama vya upinzani baada ya kuona vyama hivyo havina jipya.


No comments:

Post a Comment