21 January 2013

Askofu: Mgawanyo wa rasilimali usio wa haki unachangia vuruguNa Heckton Chuwa, Moshi

BALOZI wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Fransisco Padilla, amesema vurugu zinazotokea kwa sasa katika nchi mbalimbali duniani, zinachangiwa na mgawanyo wa rasilimali usio
wa haki katika nchi husika.


Askofu Padilla aliyasema hayo jana Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, kwenye Ibada ya Misa Takatifu, iliyofanyika
katika Kanisa la Kristu Mfalme, Jimbo la Moshi ambayo
pia ilihudhuriwa na mwenyeji wake, Askofu wa Jimbo
Katoliki la Moshi, Mhashamu Isack Amani.

Alisema rasilimali za Taifa zinapaswa kunufaisha wananchi wote lakini baadhi ya viongozi, wanakiuka utartibu huo na kuzitumia
kwa ajili ya manufaa yao ili kujinufaisha.

Aliongeza kuwa, ubinafsi ni dhambi inayotafuna dhana nzima ya wananchi wa Taifa lolote kuishi kwa amani huku wanaoendekeza ubinafsi wakinufaika na raslimali za nchi husika.

“Tamaa za namna hii huamsha hisia tofauti miongoni mwa wananchi na kujikuta wakichukua hatua za kujitetea hivyo kuharibu dhana ya kuishi kwa amani kama ilivyoelekezwa kwenye maandiko Matakatifu,”  alisema Askofu Padilla.

Alitoa wito wa Wakristo wote nchini ambao wamepewa dhamana ya uongozi katika nafasi mbalimbali kuhakikisha wanatumia maandiko Matakatifu kwa kujali ubinadamu ambapo jambo hilo litasaidia kuimarisha amani Tanzania na duniani kote.

No comments:

Post a Comment