07 January 2013
Ajali yaua,yajeruhi 21
Na Masau Bwire,Morogoro
MWALIMU wa Shule ya Msingi Ilekanilo, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Costariva Kunagar (33), amekufa na watu wengine 21 wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Chakwale,Gairo mkoani Morogoro.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro Leonard Gyindo alisema, ajali hiyo ilitokea juzi saa 11.15 jioni ikihusisha magari mawili.
Alisema kuwa gari ya moja yenye namba B 3839 aina ya Isuzu lori iliyokuwa ikiendeshwa na Nduwae Erick akitokea Dar es Salaam kuelekea nchini Burundi na
gari nyingine yenye namba T 146 CDG aina ya Toyota Coaster ikiendeshwa na Awadhi Ahmad iliyokuwa imebeba wanafamilia wakitokea Mwanza kuelekea Dar es Salaam kuhudhuria sherehe ya harusi.
Kamanda Gyindo alisema, dereva wa Toyota Coaster ambaye amevunjika mguu katika ajali hiyo alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi na alipofika eneo la tukio,gari lilimshinda kutokana na utelezi na kwenda kuvaana uso kwa uso na lori hilo.
Kamanda Gyindo alisema majeruhi 10 wamelazwa katika Hospitali ya Belega,Gairo ambapo 11 walitibiwa katika kituo cha afya Gairo na kuruhusiwa.
Alisema dereva wa Toyota Coaster ambaye ndiye inaonesha amesababisha ajali hiyo yuko chini ya ulinzi wa polisi akisubili taratibu kukamilika ili afikishwe mahakamani.
"Dereva wa Toyota Coaster Awadhi Ahmad ndiye inaonesha amesababisha ajali hiyo, amevunjika mguu na amelazwa katika hospitali ya Belega, ndugu zake wana mpango wa kumhamishia hospitali kubwa ya mifupa, nimeagiza atoe maelezo ya ajali hiyo kisha adhaminiwe na atakapopata nafuu tumfikishe mahakamani" alisema Kamanda Gyindo.
Alisema, ilikuwa wamfikishe mahakamani kesho Jumatatu ama hakimu aje kumsomea mashitaka yake hospitalini alipolazwa, lakini kutokana na mazingira na umbali wa mahakama ambayo ipo mjini Kilosa mpango huo umeshindikana.
Katika hatua nyingine, Kamanda Gyindo amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha magari yao kwa mwendo ambao hatakama likitokea tatizo katika gari haliwezi kusababisha maafa huku akiwataka baadhi ya abiria wanaowachochea madereva kuendesha kwa kasi kubwa waache tabia hiyo kwani ni hatari kwao na abiria wengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment