04 December 2012

Waziri ataja kikwazo cha utekelezaji bajeti


Na Lilian Justice, Morogoro

WAZIRI wa Fedha, Dkt. William Mgimwa, amesema kutokana na uzoefu alionao katika utumishi wa umma, amebaini bajeti nyingi za taasisi mbalimbali nchini, hazitekelezwi kwa sababu ya kukosa mipango ya utekelezaji.


Dkt. Mgimwa aliyasema hayo mjini Morogoro jana wakati akifungua Mkutano wa Nne wa Baraza la Wafanyakazi wa
Taasisi ya Uhasibu nchini (TIA).

Aliliagiza baraza hilo kutumia weledi katika kujadili uhalisia wa utekelezaji wa bajeti ambayo wataijadili kabla ya kuipitisha.

Alisema ni vyema baraza hilo likajadili namna ya kuipunguzia
Serikali mzigo wa kuchangia bajeti katika taasisi zake ili iweze kujijengea uwezo wa kushughulika na mambo mengine.

Aliongeza kuwa, katika sula la mkataba wa hali bora dhumini lake
ni kutoa nafasi ya kuridhiana kikazi kwa mfanyakazi kutimiza wajibu wao na mwajiri kutoa haki na masilahi kwa mfanyakazi.

Dkt. Mgimwa alisema, suala la uwajibikaji na mahusiano mema mahali pa kazi ni jambo kubwa linalohitaji mjadala mpana kwani limekuwa na matokeo chanya au hasi mahali pengi pa kazi hasa katika taasisi za umma.

“Wafanyakazi mnapaswa kuwa waaminifu, hivi sasa dunia ipo katika utandawazi hivyo baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakitumika katika kuvujisha taarifa za ndani kwa watu wasiohusika, hali hii inapaswa kukemewa kabla haijaleta madhara,” alisema.

Alitoa wito kwa viongozi sehemu za kazi, kutatua migogoro kwa njia za kisheria, taratibu, kusisitiza busara na hekima itumike wakati wa kutekeleza sheria hizo kwa wafanyakazi ambao watabainika kuwa na makosa kazini.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Shah Hanzuruni, alisema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na taasisi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka hivyo taasisi imeanzisha tawi jingine jijini Mwanza.

“Hadi sasa tuna matawi matano ambayo moja lipo mkoani Mbeya, Singida, Mtwara na Mwanza,” alisema Hanzuruni.

Alisema mwaka huu wa fedha, taasisi hiyo inaanza mchakato wa kuanzisha tawi lingine mkoani Kigoma, ambapo idadi ya wanafunzi waliodahiliwa ngazi ya cheti, stashahada, shahada na stashahada ya juu ambao wanaendelea na masomo wapo 12,235 ambapo mwaka 2013/14 wanatarajia kuwa na wanafunzi 12,891.


No comments:

Post a Comment