Darlin Said na Gift Mongi
WASICHANA waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu wamefanya vizuri ambapo jumla ya wasichana 281,460 sawa na asilimia 50.20 wamefaulu ikilinganishwa na wavulana 279,246 sawa na asilimia 49.80 waliofanya mtihani.
Akitoa matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt Shukuru Kawambwa alisema jumla ya watahiniwa 865,827 sawa na asilimia 96.76 walisajiliwa kufanya mtihani huo.
Alisema kati ya hao wasichana 456,082 sawa na asilimia 52.68 walifanya mtihani wakati wavulana walikuwa 409,745 sawa na asilimia 47.32.
"Matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yanaonesha kuwa alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana,"alisema Dkt.
Alisema matokeo hayo yanaonesha jumla ya watahiniwa 3,087 walipata alama za daraja 'A' wakati wanafunzi 40,683 daraja 'B' na jumla ya wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja 'C'.Wanafunzi 526,397 'D' na watahiniwa 73,264 walipata alama 'E' ambayo ni ya mwisho.
Aidha alisema jumla ya wanafunzi 560,706 kati ya 865,534 ambao sawa na asilimia 64 ya waliofanya mtihani huo wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
"Takwimu zinaonyesha idadi ya wananfunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari imeongezeka kwa asilimia 8.8 ukilinganishwa na wanafunzi 515,177 waliochaguliwa mwaka jana," alisema Dkt.Kawambwa.
Katika hatua nyingine Dkt. Kawambwa alisema kwa mwaka huu udanganyifu umepungua tofauti na miaka ya nyuma kwani watahiniwa 293 ndio waliofutiwa mitihani ikilinganishwa na 9,736 waliofutiwa mwaka jana.
Alisema kupungua kwa udangavyifu huo imetokanana na watahiniwa hao kutumia teknolojia mpya maarufu kama 'Optical Mark Reader(OMR)' ambapo mitihani ilisaishwa kwa kutumia komputa.
"Lakini pia nikiri kwamba teknolojia hii imesaidia katika zoezi la usaishaji kwani imepunguza upotevu mwingi wa muda pamoja na serikali kutumia walimu wachache tofauti na miaka ya nyuma ambapo kwa mwaka huu walimu waliotumika kusaisha walikuwa 285 kwa muda wa siku 15 wakati kipindi cha nyuma walitumika walimu zaidi ya4,000 kwa muda zaidi ya mwezi," alisema.
Kuhusu ufaulu wa shule za serikali zimefanya vizuri ikilinganishwa na za binafsi ingawaje hata hizo zimefanya vizuri na hii inatokana na kwamba idadi ya shule za serikali ni 16,331 idadi ambayo ni kubwa ikilinganisha na za binafsi ambazo ni chache kwa upande wa shule za msingi.
Akizungumzia kuhusu wanafunzi kuingia kidato cha kwanza bila kujua kusoma na kuandika alisema, Wizara imeandaa mkakati wa kuwapa mtihani ili kubaini wale wote wasiojua kusoma na kwamba ikiwa watagundulika watasaidiwa kwa namna nyingine pamoja na kufutiwa usajili wao.
Hata hivyo Dkt.Kawambwa alisema jumla ya wanafunzi 894,839 walisajiliwa kufanya mtihani ambapo wasichana walikuwa 468,583 sawa na asilimia 52.37 na wavulana 426,256 sawa na asilimia 47.63.
Alisema kati ya hao watahiniwa 29,012 sawa na asilimia 3.24 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ukiwamo utoro, vifo na ugonjwa na kwamba wasichana walikuwa 12,501 sawa na asilimia 2.67 na wavulana 16,511 sawa na asilimia 3.87.
No comments:
Post a Comment