21 December 2012

Wapelelezi kuchunguza madai polisi kuiba mil. 150/-



Leah Daudi na Zubeda Mazunde

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limeunda
jopo la wapelelezi ili kuchunguza taarifa zinazodai sh. milioni
150 zilizoibwa na majambazi kwenye tukio la ujambazi ambalo lilitokea hivi karibuni katika Mtaa wa Mahiwa na Livingston, Kariakoo, Dar es Salaam, ziliibwa na kupotelea mikononi mwa polisi ambao walihusika kuwakamata watuhumiwa.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 18 mwaka huu.

Alisema jopo hilo limeundwa ili kujiridhisha na habari ambazo zimeandikwa na baadhi ya vyombo vya habari juu ya baadhi ya
polisi kuhusika na wizi wa fedha hizo.

“Habari hizo zilisisitiza kuwa, polisi waliochukua fedha hizo walikwenda kugawana eneo la Jangwani, mimi na wenzangu
tumezichukulia taarifa hizi kwa uzito mkubwa na kuona bora
uchunguzi wa kina ufanyike ili kuthibitisha tuhuma hizi.

“Jopo la wapelelezi litakuwa na watu watano likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Ahmed Msangi na matokeo ya uchunguzi huo yatatolewa kwa wananchi,” alisema Kamanda Kova.

Aliongeza kuwa, kama itabainika tuhuma hizo zina ukweli, wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria na ili kufanikisha uchunguzi huo, anawaomba watu wenye taarifa sahihi wajitokeze
ambapo jeshi hilo litawalinda na kutunza siri zao.

Alisema wale waliokuwepo wakati watuhumiwa hao wakikamatwa, nao wajitokeze ili kueleza jinsi walivyoshuhudia tukio hilo na kubaini kama polisi waliondoka na kielelezo chochote ambacho kinadaiwa ni fuko la fedha kama ilivyoelezwa.

“Wale wanaofahamu eneo la Jangwani au nyumba ambayo polisi waliitumia kugawana fedha hizi nao wajitokeze ili wasaidie kubaini ukweli wa tukio hili kwa uongozi wa Jeshi la Polisi siku zote unasisitiza utendaji mzuri, nidhamu uaminifu na weledi.

“Kama ofisa au askari atakiuka maadili ya kazi yake, atachukuliwa hatua bila kuchelewa na yule anayefanya mazuri, atazawadiwa” alisema Kamanda Kova.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanikiwa kukamata risasi 200 za bunduki aina ya SMG, kwenye msako wa kuwatafuta watu wawili waliokuwa katika pikipiki baada ya kupokea taarifa kutoka kwa msiri.

Silaha hiyo na risasi zake vimepatikana Desemba 19 mwaka huu, Kimara Mwisho, baada ya msiri kufikisha taarifa Kituo cha Polisi Mbezi, kilichopo Mkoa wa Kipolisi Kinondoni.

“Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kimara, aliongozana na polisi kwenda Kimara Mwisho na walipokaribia eneo la tukio, waliwaona watu wawili wakiwa na pikipiki ambayo namba zake hazikusomeka wakiwa na begi.

“Wakati askari wakijipanga kuwakamata, watu hao walishtuka, kutupa begi na kukimbia kwa kutumia pikipiki waliyokuwa nayo,” alisema Kamanda Kova.

Aliongeza kuwa, polisi walichukua begi hilo na baada ya kulikagua, walikuta risasi 200 za bunduki aina ya SMG, ambapo jitihada za kuwatafuta watuhumiwa na pikipiki yao zinaendelea.

No comments:

Post a Comment