21 December 2012

Wanawake CUF wapewa mbinu ya ushindi



Na Mwandishi Wetu,Tanga

CHAMA cha Wananchi(CUF)kimewahimiza wanawake wa Jumuiya ya Chama hicho kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao ili kujenga jumuiya yenye nguvu itakayowezesha kupatikana kwa ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.


Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo ya chama hicho Taifa,Nuru Awadh Bafadhili alisema umoja na mshikamano miongoni mwa wanawake ndio nguzo pekee ya ushindi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Aliwataka kutokubali kununuliwa kwa vitu vidogo kama vile kanga na vilemba hasa nyakati za uchaguzi badala yake waunganishe nguvu ya pamoja itakayowezesha kukiondoa madarakani chama cha Mapinduzi.

Bafadhili alisema ushindi wa Chama hicho unawategemea zaidi wanawake na kusisitiza kama wataendelea kushikamana ni wazi kuwa watafanikisha azma ya CUF kuingia madarakani mwaka 2015 kwani ndicho chama chenye dhamira ya dhati ya kuwaletea mabadiliko  ya kweli wananchi.

Alisifu juhudi kubwa zinazofanywa na wanawake katika kukijenga chama hicho na kusisitiza kuwa kazi waliyoianza katika mikoa mbalimbali hawana budi kuindeleza hadi uchaguzi mkuu ujao ili kufanikisha lengo la chama hicho kushika dola.

Alisema kwa muda mrefu sasa CCM imekuwa ikiwatumia wanawake kama daraja la kuwaingiza madarakani lakini baada ya hapo huwatupa na kushindwa kujali adha zinazowapata kama huduma za afya na maji ambazo zimekuwa zikiwaathiri zaidi wanawake.

Katibu huyo Mtendaji wa Jumuiya hiyo aliwahimiza wanawake kote nchini kukataa kutumika kufanikisha malengo ya wengine badala yake waungane pamoja kupata safu mpya za uongozi utakaowajali hasa wanawake  ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakidhalilika kupata huduma muhimu za kijamii.

No comments:

Post a Comment