21 December 2012

Wafanyakazi TAZARA wagoma tena


Na Rehema Maigala

WAFANYAKAZI wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), jana wameanza mgomo mwingine wa kutofanya
kazi hadi Serikali itakapowalipa mishahara ya miezi mitatu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (TRAWU) Taifa, Bw. Erasto Kihwele, aliyasema hayo katika mkutano wafanyakazi wa shirika hilo.

Mkutano huo ulilenga kujadili hatma ya mishahara yao ya Oktoba, Novemba na Desemba mwaka huu hivyo kusababisha washindwe kuhudumia familia zao.

“Hatuwezi kufanya kazi katika mazingira magumu, treni ambazo tunaziendesha huwa tunapakia roho za watu na mizigo yenye thamani kubwa hivyo tunaweza kusababisha ajali hivyo Taifa
kupata hasara kubwa,” alisema Bw. Kihwele.

Alisema hivi sasa wafanyakazi wa shirika hilo wameota meno ambapo kipindi cha nyuma walikuwa kibogoyo hivyo hawapo
tayari kufanya kazi hata wakiombwa na Waziri Mkuu kama
hawatalipwa mishahara ya ya miezi mitatu.

“Stesheni zote za TAZARA zimesimamisha kazi ili kujua hatma ya mishahara ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya na Mrimba ambao nao wamekutana leo (jana)  kuzungumzia jambo hili,” alisema.

Mwenyekiti wa TRAWU Taifa, Bw.  Musa Kalala, alisema inasikitisha kuona baadhi ya wafanyakazi hawana umoja
hivyo kuzorotesha nguvu ya wafanyakazi.

“Umoja ni kitu kizuri na daima kinazaa kitu chema lakini wafanyakazi wanaotengeneza mabehewa (kalakana), wameosha udhaifu wa kutogoma baada ya kuahidiwa sh. 100,000.

“Hadi sasa wanaendelea na kazi pamoja na kutolipwa mishahara
yao ya miezi mitatu sijui yutawasaidiaje,” alisema Bw. Kalala.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo katika mkutano walisema hawapo tayari kufanya kazi yeyote hadi watakapolipwa stahiki zao za miezi mitatu si vinginevyo.

“Safari hii hatutaki ahadi wala mshahara wa mwezi mmoja, tutaingia ofisini asubuhi, kusaini kitabu cha mahudhurio na kukaa kwenye ukumbi wa mkutano kujadili madai yetu, ikifika jioni tutaondoka hadi kieleweke,” walisema wafanyakazi hao.

Novemba mwaka huu, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Bw. Charles Tizeba, alifanya kikao kilichoshirikisha uongozi wa TAZARA na TRAWU ili kujadili mishahara ya wafanyakazi.

Katika kikao hicho, Bw. Tizeba aliuagiza uongozi wa TAZARA uwalipe wafanyakazi stahiki zoa haraka iwezekanavyo lakini hadi
jana agizo hilo lilikuwa halijatekelezwa.

1 comment:

  1. msijadiri mpewe mishara mitatu jadirini viongozi wanaosababisha mkose mishara waondolewe na serikali itowe hera kwa sababu imewaweka yenyewe
    mtadai mishara hadi lini?

    ReplyDelete