03 December 2012

Udhibiti majitaka viwandani unasaidia kutunza mazingira



Na Mwandishi wetu

VIWANDA ni moja ya sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi kutokana na kwamba bila sekta hiyo kuimarika taifa huathirika kimapato na kushindwa kuboresha miundombinu mbalimbali na ustawi wa jamii.


Viwanda huongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika nchi kwa lengo la kupata masoko zaidi ya ndani na nje ya nchi ambapo kwa kufanya hivyo taifa linakuwa limepiga hatua katika maendeleo.

Wakati jitihada za kuifanya sekta ya viwanda inapiga hatua katika uzalishaji, pia sekta hii ina wajibu wa kuhakikisha uzalishaji huo hauathiri mazingira kutokana na kwamba mazingira ni moja ya nguzo muhimu katika maendeleo endelevu.

Sekta ya viwanda hutumia maji wakati wa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na huzalisha maji taka ambayo huwa na athari kwa ardhi, viumbe hai na maisha ya binadamu kama kiwanda hakikuchukua hatua stahiki katika kuhakikisha majitaka hayo hayaleti madhara pindi yanapomwagwa kwenye mazingira.

Viwanda vinatakiwa viwe na mikakati ya kupunguza matumizi makubwa ya maji ili kulinda rasilimali hiyo na pia kujenga miundombinu ambayo itasaidia kuyatibu majitaka yatakayozalishwa hadi kufikia viwango vinavyoruhusiwa kabla ya kutiririshwa kwenda katika mito na mabonde na vyanzo vya maji na mazingira.

Meneja Mradi wa Shirika lisilo la Serikali ENVICON, Evody Ndumiwe anasema taasisi yao ni moja ya taasisi iliyotambua kuwepo kwa tatizo la uharibifu wa mazingira pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji unaotokana na shughuli za uzalishaji viwandani.

Kutokana na kuwepo kwa tatizo hilo, ENVICON kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendesha mradi wa kujenga uwezo juu ya Mfumo wa Usimamizi wa Mazingira, (EMS) kwa wenye viwanda na wafanyakazi katika jitihada za kuboresha usimamizi wa mazingira ili kudhibiti uharibifu mazingira utokanao na shughuli za viwanda.

Anasema viwanda vinahitajika kuhakikisha maji taka yenye madhara yeyote hususani kemikali yanatibiwa kabla yajatiririshwa kwenye mito na mabonde ili yasilete  madhara makubwa kwa viumbe, ardhi, wanyama na binadamu ambao huyatumia kwa ajili ya kunywa, kupikia na matumizi mbalimbali ya nyumbani.

Anasema ENVICON kwa sasa inafanya kazi na viwanda vitano vilivyopo katika Bonde la Mto Ruvu-Wami kuwasaidia kuanzisha EMS ndani ya mradi mkubwa wa Maji na Maendeleo awamu ya pili.

Mradi huo unajulikana zaidi kwa jina la Water and Development Alliance  (WADA II)  ambao  ni mradi wa miaka mitatu ambao umejikita katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira pamoja na kulinda na kuhifadhi rasilimali maji.

Viwanda hivyo vitano ni 21st Century Textile Mills, Tungi Sisal Estate, Kibaha Tannerry, Mtibwa Suger Estate, na Machinjio ya Dodoma (Dodoma Abattoir)

EMS ni utaratibu wa kina wa usimamizi wa masuala ya mazingira, unaounganisha mtazamo wa mazingira na shughuli zote za usimamizi wa uzalishaji viwandani unaolenga kusimamia na kuhusisha mipango yote ya usimamizi wa kiwanda na suala la mazingira.

Pia inasaidia kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipau mbele pamoja na masuala mengine kama gharama, ubora wa bidhaa, uwekezaji na mipango. Ni nyenzo muhimu ya kuzuia athari zitokanazo na shughuli za viwanda kwa mazingira.

“Kazi yetu kubwa katika mradi huu ni kuwaelimisha viongozi wa viwanda na wafanyakazi njia za kupunguza matumizi ya maji, na kusimamia rasilimali maji isiweze kuharibiwa kutokana na maji taka yatokayo viwandani,” anasema Evody.

Kwa kiasi kikubwa mpango huu umefanikiwa kuwaelimisha wenye viwanda umuhimu na faida za kuanzisha na kutekeleza mfumo wa usimamizi wa mazingira kwenye viwanda vyao.

Viwanda hivyo vimeunda kamati zitakazosimamia masuala yote ya mazingira na pia vimeshatengeneza mipango kazi kwa ajili ya kuboresha hali ya usimamizi wa mazingira viwandani kwa hiyari yao wenyewe.

Anasema kuwa viwanda vikitekeleza vizuri mfumo wa usimamizi wa mazingira vinaweza kupunguza matumizi ya rasilimali ikiwamo maji na kupunguza uzalishaji wa taka wakati huo huo vikiongeza uzalishaji wao.

Kwa kufanya hivyo viwanda vitakuwa vimesaidia katika kuhifadhi rasilimali maji yanavyotegemewa kwa matumizi ya binadamu na viumbe hai vingine  vya majini.

Mhandisi Mazingira Ofisi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Morogoro, Abdhallah Mshana anasema uchafuzi wa maji katika Bonde la Wami- Ruvu unatokana na viwanda vingi ambavyo hutiririsha maji taka ambayo hayakizi vigezo vya kimazingira jambo ambalo ni hatari kwa viumbe hai wa majini na binadamu.

Anasema eneo la Kihonda viwandani kuna mabwawa ya kutiba majitaka yaliyojengwa na serikali ambayo kwa sasa hayatumiki hivyo majitaka yanayotoka viwandani hutiririka kuelekea Mto Ngerengere na kusababisha madhara ya kiafya na kimazingira.

Mabwawa hayo yalijengwa kwa ajili ya kutibu majitaka yanayozalishwa na viwanda vilivyopo eneo hilo. Kwa sasa mabwawa hayo yametelekezwa na pia maeneo yaliyopo karibu yamevamiwa na wananchi ambao wameanzisha makazi.

Uongozi wa Bonde Wami-Ruvu unaendelea kutafuta vibali kutoka mamlaka nyingine za serikali ili kuweza kuyamiliki mabwawa hayo na kuyafanyia ukarabati kwa ajili ya maji taka kutoka katika viwanda hivyo kwa lengo la kuzuia maji taka kwenda katika Bonde hilo ambalo ni muhimu kwa viumbe na maji yanyotumiwa na miji ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.   

Katika bonde hilo maji hutumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za binadamu, mifugo na kwa ajili ya viumbe wa majini hivyo madhara yake ni makubwa kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kuhakikisha uchafuzi wa viwandani zikiwemo kemikali hatarishi zote zinatibiwa hadi kufikia viwango vinavyoruhusiwa.

Afisa mwandamizi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Programu ya iWASH na WADA, Vincent Vyamana anasema mazingira ni kitu muhimu katika taifa hivyo kuna kila sababu serikali na wadau wa mazingira kwa pamoja kushiriki kuhakikisha yanabakia kuwa salama wakati wote.

Anasema ni lazima vyanzo vya maji vilindwe na kutunzwa, miti haikatwi ovyo, na shughuli za viwanda kutokuwa sehemu ya uharibifu wa mazingira ili kusaidia nchi kuwa katika hali ya usalama kutokana na kwamba hali siyo nzuri katika mstakabali wa maisha ya binadamu, viumbe na rasilimali mbalimbali.

Anasema taasisi za serikali zinazohusiaka na utekelezaji wa sheria ni lazima zitekeleze wajibu wao na wadau wengine wa mazingira kutoa elimu ili kuzuia vitendo vinavyo hatarisha usalama wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini likiwemo bonde la Ruvu-Wami ambalo maji yeke yanatumika na watu wengi na mifugo.

Sheria za mazingira ni lazima zifanye kazi na taasisi kama Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wadau wengine serikali wasikae tu katika ofisi zao bali wajenge utamaduni wa kwenda kukagua maeneo mbalimbali yakiwemo ya viwanda na vyanzo vya maji kuhakikisha mazingira yanakuwa salama wakati wote.

Wafanyabiashara wengi katika shughuli zao wanachoangalia ni kupata faida hata kama atakuwa anafahamu anachokifanya kinahataraisha mazingira hivyo ni jukumu la mamlaka kupita na kuwakumbusha wamiliki kuhakikisha suala hilo linakuwa la kipaumbele katika shughuli zao za uzalishaji.

Mara nyingi tunaona kuwa sheria zipo lakini utekelezaji unakuwa ndiyo tatizo katika kufikia malengo hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha jambo hili linafanikiwa kwa kutimiza malengo kwa kila upande yani wenye viwanda, serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kushiriki kikamilifu.

Utamaduni huo ukijengwa na wenye viwanda kwa kutoa kipaumbele kwa mazingira kuwa katika hali ya usalama  itasaidia kulinda viumbe, vyanzo vya maji na uhai wa binadamu kutokuwa katika hatari ya kukumbwa na matatizo.


No comments:

Post a Comment