20 December 2012
TEMESA kukarabati Kivuko Kilombero
Na Severin Blasio, Kilombero
WAKALA wa Ufundi na Umeme(TEMESA) Mkoa wa Morogoro wameahidi kukifanyia matengenezo ya haraka kivuko M.V Kilombero I ili kitumike kuvushia mitambo na magari mazito yatakayotumika kujengea daraja kuu la mto Kilombero wakati kivuko M.V Kilombero II kikielekezwa kuvusha abiria na magari ya kawaida.
Akizungumza katika kikao cha sita cha bodi ya ushauri ya Kivuko cha Mto Kilombero,Kaimu meneja wa TEMESA mkoa wa Morogoro ,Mhandisi Magreth Mapela alisema njia ya kukifanyia ukarabati kivuko hicho cha mwanzo itarahisisha utendaji wa kazi kwa pande zote mbili kwa ufanisi bila kuingiliana na kusumbua wananchi.
Aidha kwa mujibu wa Mapela mbali na matengenezo hayo pia kutakuwa na mabadiliko ya muda wa kufanya kazi kutoka kuishia saa 1.30 jioni hadi saa 4 usiku katika kipindi chote cha ujenzi wa daraja ili kupunguza msongamano wa magari ya abiria na mizigo.
Kaimu meneja huyo alisema mpango kazi wa mwaka 2012/13 unatarajia kukusanya shilingi Milioni 808,120,800 zitakazotumika kulipia mishahara,mafuta,posho, matengenezo ya kawaida,dharura na kulipia madeni.
katika ukarabati wa vivuko Kaimu Meneja huyo alisema kuwa wanatarajia kukamilisha ukarabati wa vishikio vya mwisho vya lango la kivuko cha M.V Kilombero II(Flaps) na sehemu zote chakavu kazi itakayokuwa imekamilika kabla ya Arili 2013.
Hata hivyo Kaimu meneja huyo ametaja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni utobokaji wa mara kwa mara wa tenki la vivuko unaosababishwan na kujisugua kwenye maegesho ya kivuko(gati)ambayo kwa sasa inakarabatiwa,ukosefu wa sehemu za kupumzikia abiria ambapo husababisha adha kubwa kipindi cha mvua na jua kali.
Nyingine ni ajali za magari kugonga kivuko na kutumbukia majini kutokana na ubovu wa mfumo wa breki za magari hayo,majani na nyavu kusonga mfumo wa usukani wa kivuko na kusababisha mara kwa mara kivuko kusimama ili kuondoa majani na nyavu.
Kwa upande wake Katibu tawala wa mkoa wa Morogoro Eliya Ntandu aliyekuwa mgeni rasmi alisema mbali na kutokuwepo hoja juu ya vivuko hivyo katika wilaya zote mbili elimu ya uokoaji inahitajika ili wananchi waweze kujikinga kabla ya janga kutokea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment