20 December 2012

Tatizo la maji Songea ni kero inayoendelea kuwatesa wakazi wa mji huo


Na Kassian Nyandindi


KIUMBE chochote kilicho hai duniani, asilimia kubwa ya maisha yake huendeshwa kwa kutumia maji, hivyo basi ni kitu muhimu na jambo ambalo halina mjadala.

Endapo kunakuwa na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kunaweza kusababisha matatizo mengi katika jamii, yakiwemo magonjwa ya mlipuko na maji  hayo yanapopatikana kwa shida hugeuka na kuwa karaha.

Serikali imekuwa ikisisitiza wakati wote jamii kutunza mazingira ikiwemo vyanzo vya maji ambavyo ndio mhimili mkuu wa upatikanaji wa maji ambayo humsaidia binadamu kuendesha maisha yake.

Tatizo la upatikanaji wa maji na uharibifu wa vyanzo vya maji, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, umefanywa na watu wachache ambapo hivi sasa imekuwa ni kero kubwa ya upatikanaji wa nishati hiyo muhimu.

Uhaba wa maji katika manispaa hiyo ni tatizo ambalo limekuwa likiendelea kutesa wakazi wa Songea kutokana na vyanzo vya maji ambavyo vimekuwa vikizalisha nishati hiyo muhimu kuanza kupoteza uwezo wake wa kuzalisha maji kwa wingi.

Maeneo mengi ya mji huo kwa sasa yanakosa huduma ya maji safi kwa asilimia 69 ya mahitaji ambapo maji yanayozalishwa ni wastani wa mita za ujazo 3000 kwa siku, wakati mahitaji halisi ni meta za ujazo 9700 kwa siku.

Mhandisi wa mipango na ujenzi Jaffary Yahaya anasema mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (SOUWASA) katika manispaa ya Songea inategemea vyanzo tisa vya maji ambavyo ni chemchem, vilivyopo katika mlima Matogoro kuzalisha maji kwa ajili ya watumiaji.

Anasema upungufu mkubwa wa maji katika vyanzo hivyo, umekuwa ukijitokeza hasa kipindi cha kiangazi ambapo maji yanayopatikana ni asilimia 31 tu kwa siku jambo ambalo linasababisha kuwepo na mgawo mkali wa kusambaza maji katika makazi ya watu au taasisi mbalimbali.

Anaeleza kwamba vyanzo vya maji vilivyopo sasa vina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya wakazi wa manispaa hiyo hadi mwishoni mwa mwaka huu, na baada ya hapo vyanzo vingine vinatakiwa kujengwa ili kuondokana na adha hiyo iliyopo sasa.

“Hadi sasa usanifu na makadirio ya ujenzi wa miundombinu mipya ya maji umekwisha fanywa na kuwasilishwa wizara ya maji, lakini upatikanaji wa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo (WSDP) nib bado hadi leo hii”, anasema.

Anabainisha kwamba mtandao wa maji safi upo sehemu ndogo ya manispaa ya Songea, ambapo upo katika eneo la asilimia 56 na bado asilimi 44 ambayo haina mtandao wa maji hayo.

Anafafanua kuwa tatizo la uhaba wa maji linachangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa vyanzo vya maji vilivyoko katika milima Matogoro, kutokana na uchomaji moto misitu ya asili na shughuli za kibinadamu zisizo rasmi katika hifadhi ya vyanzo vya maji, hivyo kupunguza kiasi kikubwa cha maji yanayoweza kupatikana kutoka vyanzo vya chemchem.

Hali hiyo hupunguza kiasi kikubwa cha maji yanayoweza kupatikana kutoka vyanzo vya chemchem vilivyopo katika milima hiyo, pamoja na maji ya kutoka mto Luhira ambayo baadae husukumwa kwa pampu maalum.

Upungufu wa maji umeendelea kuathiri viwango vya utoaji wa huduma ya maji safi, hivyo wateja waliounganishiwa bomba na wanaoishi kwenye maeneo ya mgandamizo mdogo wa maji, hawapati nishati hiyo ipasavyo kutokana na usanifu wa mfumo wa usambazaji maji kuwekwa kwenye kanda za usambazaji na kutegemea uwepo wa maji mengi katika tenki la usambazaji kwa kanda husika.

Maeneo yenye mwinuko wa juu kama vile Makambi, Mateka, Songea mjini, Majengo na Bombambili yamekuwa yakikumbwa na adha hiyo mara kwa mara.

Anasema hadi sasa bomba zilizolazwa katika mfumo wa maji safi zina jumla ya urefu wa kilometa 287 zenye kipenyo kati ya milimita 75 hadi 400 na kwamba mtandao wa bomba hizo upo katika wastani wa asilimia 56 kwa eneo la manispaa hiyo.

Kwa upande wa mtandao wa maji taka una jumla ya urefu wa kilometa 37, mabwawa sita yamejengwa kwa ajili ya shughuli za kutibu maji taka.

Anasema wateja waliounganishiwa mfumo huo ni 1,010 kati ya 1500 waliolengwa kuunganishiwa ifikapo Juni 2013 kwa kutumia mtandao wa majitaka pamoja na maabara iliyopo ambayo hutumika katika kuyasafisha maji hayo na kuyatibu kabla ya kuwafikia watumiaji.

Changamoto nyingine inayokabiliana nayo mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira katika manispaa ya Songea ni kwamba taasisi za serikali kutolipia ankra zao za maji kwa wakati ambapo hali hii husababisha mamlaka hiyo kudai deni la shilingi 209,000,000.

Kutokana na tatizo hilo uwezo wa mamlaka kugharimia shughuli za uendeshaji na matengenezo umepungua, hivyo kusababisha wafanyakazi, wazabuni na wadau mbalimbali kuidai mamlaka kwa kiasi kikubwa cha fedha.

Pamoja na mambo mengine hatua zilizochukuliwa katika juhudi za kutatua kero hii ya upatikanaji wa maji, mamlaka hiyo kwa kutumia fedha za makusanyo ya maduhuli imeweza kujenga bwawa dogo lenye uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo 13,000 kwa gharama yashilingi milioni 15.2.

Hata hivyo bwawa hilo dogo ikilinganishwa na mpango uliopo wa kujenga bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo 1,000,000 ambalo litagharimu dola milioni 1,264,004.

Pamoja na mambo mengine hatua zilizochukuliwa katika juhudi za kutatua kero hii iliyopo sasa na baadhi ya changamoto zilizopo ni kwamba, mamlaka hiyo kwa kutumia fedha za makusanyo ya maduhuli imeweza kujenga bwawa dogo lenye uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo 13,000 kwa gharama ya shilingi milioni 15.2.

Hata hivyo bwawa hilo ni dogo, ikilinganishwa na mpango uliopo wa kujenga bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo 1,000,000 ambalo litagharimu dola milioni 1,264,004.



No comments:

Post a Comment