20 December 2012

Serikali iwapige marufuku waganga wanaojiita 'lambalamba'-Wataalamu


Na Grace Ndossa

UONGOZI wa Serikali mkoani Dodoma, umeombwa kuwapiga marufuku watu wanaojiita waganga wa kienyeji maarufu kama 'lambalamba', ambao wanajifanya kutoa uchawi katika makazi
ya watu ili wasiweze kuhatarisha amani na utulivu uliopo.

Ombi hilo limetolewa juzi na Mwenyekiti wa Baraza la Waganga
wa Tiba Asili, Bw. Shaka Mohamed, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya wimbi la watu wanaojiita waganga
mkoani humo na kudai kutoa uchawi.

Alisema viongozi wa dini nao wana jukumu la kukomesha vitendo hivyo na kutoa elimu kwa jamii ili iondokane na mawazo mgando
ya kuwaamini watu hao na kuwapa pesa zao za mavuno.

“Hawa lambalamba huwa wanaonekana katika msimu wa mavuno wakijua wananchi wana fedha hivyo dhamira yao ni kuwadhurumu, kuwatia umaskini na kutaka kuvuruga amani iliyopo,” alisema.

Aliongeza kuwa, kama watu hao wataendelea kufanya shughuli zao bila Serikali kuchukua hatua, upo uwezekano mkubwa wa amani na utulivu uliopo mkoani humo kuvunjika.

“Mauaji ya albino na vikonge yanaweza kuibuka tena kutokana na imani zilizojengeka miongoni mwa wananchi na mwisho wa siku, watauana wenyewe kwa wenyewe kutokana na uadui ambao utakuwa umejengwa na hawa waganga,” alisema Bw. Mohamed.

No comments:

Post a Comment