20 December 2012

Dar yaongoza kwa rushwa *Sekta ya afya yadaiwa kushika namba moja *Utafiti wafichua siri za wabunge majimboni



Na Rehema Maigala

ASILIMIA 60 ya wakazi wa Dar es Salaam, wamesema vitendo
vya rushwa mkoani humo vimeongezeka kwa kasi kubwa tofauti
na miaka mitano iliyopita.


Utafiti huo umefanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza ambayo ilikusanya maoni mbalimbali ya wakazi wa Mkoa huo yanayohusu huduma, Sera na utendaji kazi wa viongozi.

Akitoa ripoti ya miaka miwili kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtafiti kutoka taasisi hiyo, Elvis Mushi, alisema
idadi kubwa ya watu walisema wanalazimika kutoa rushwa ili kupata huduma iliyopaswa kutolewa bila malipo katika
vituo vya afya.

Alisema wananchi hawaridhishwi na mazingira ya utoaji huduma za jamii kama afya, maji, miundombinu ya barabara pamoja na umeme.

“Wananchi walipoulizwa juu ya imani waliyonayo kwa taasisi za umma walisema Mahakama na Jeshi la Polisi wanafanya kazi zao vizuri kuliko Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASCO) na kudai inafanya kazi kwa upendeleo.

“Karibu nusu ya wakazi wa jiji hili, hawajui majina ya wabunge hao, hii inatokana na wabunge wenyewe kutowatembelea wananchi
mara kwa mara hadi kipindi cha uchaguzi,” alisema.

Aliongeza kuwa, asilimia 70 ya wananchi ambao walihojiwa, walisema hawakuwahi kusikia na kushindwa kutafsili maana
ya MKUKUTA, Kilimo Kwanza na Jumuiya ya Afrika
Mashiriki.

No comments:

Post a Comment