20 December 2012
Mahakama yampa agizo RC Moro
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi jijini Dar es Salaam, imemtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Joel Bendera
na watendaji wengine, kusitisha uhamishaji wananchi
waishio katika Bonde la Kilombero na Ulanga.
Uamuzi huo ulitokana na Mahakama hiyo kutoa zuio Novemba 21 mwaka huu la kuitaka Derikali kuacha kubomoa nyumba za wakazi 1,994, kuwahamisha wafugaji na mifugo yao katika vijiji 50 katika bonde hilo hadi kesi ya msingi itakapotajwa.
Akitoa agizo hilo maahakamani hapo jana, Jaji Atuganile Ngwala, alidai hatua ya Bw. Bendera, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Hassan Masala, Ofisa wa Polisi, Bw. Aloyce Nindi, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Bw. Francis Nditi na Ofisa wa Polisi Ulanga,
Bw. Abeid Fanje kukaidi agizo la Mahakama ni kinyume na
taratibu za kisheria.
Kesi hiyo yenye namba 212/2012, ilifunguliwa Oktoba 31 mwaka huu na walalamikaji Godfrey Luena, Zablon Mkwage, John Masele na Elia Mtupili na wenzao 2019 dhidi ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ya kupinga kuondolewa katika eneo hilo bila ya kulipwa fidia.
Alisema kutokana na viongozi hao kuvunja sheria, wanapaswa kufika mahakamani ili kujibu tuhuma hizo.
Hata hivyo, hati ya kuwaita mahakamani ilitolewa Desemba 17-18 mwaka huu, ambayo iliwasilishwa kwa wahusika kupitia madalali wa Mahakama.
Wananchi hao wamehamishwa kwenye eneo hilo ili kupisha mradi wa uhifadhi wanyama pori unaojulikana kwa jina la 'Ramsey'.
Katika kesi hiyo, wananchi hao wamefungua shauri la kupinga kuondolewa katika maeneo hayo bila ya kulipwa fidia wakisaidiwa na wanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Kwa upande wake, Bw. Bendera alipohojiwa alisema lengo la kuwaondoa wananchi hao ni kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wananchi kuharibu vyanzo vya maji na ukataji misitu hovyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment