24 December 2012

Pongezi TBS kwa kufichua uozo wa kondomu za Melt Me



SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetangaza kuzipiga marufuku kondomu za Melt Me, kutokana na kuingizwa nchini kwa njia za panya, huku zikiwa hazikidhi ubora wa viwango.

Tayari shehena ya kondomu hizo ilikuwa imezuiwa bandarini baada ya kubainika hazikidhi viwango huku taratibu za kurejeshwa zilikotoka nchini India zikiendelea.

Wakati taratibu hizo zikiendelea wakaguzi wa shirika hilo, walibaini kuwepo kwa kondomu za aina hiyo madukani, hivyo walilazimika kurudi bandarini kujiridhisha kama shehena iliyozuiwa na maofisa wake, ndiyo hiyo imeingizwa kwenye soko kiujanja.

Hata hivyo shehena hiyo ilikutwa bado ipo bandarini, hali inayodhihirisha kuwa kondomu hizo zimeingizwa kwenye soko kwa njia za panya. Hali hiyo imelifanya shirika hilo kupitia Kaimu Mkurugenzi wake, Bw. Leandri Kinabo, kutaka wananchi kuacha kutumia kondomu hizo kwani si salama.

Kwa mujibu ya maelezo ya kitaalam ya maofisa wa TBS, kondomu hizo zikiwekwa maji yanapita na zikiingizwa hewa zinapasuka kabla ya kufikia kiwango kinachotakiwa hali inayodhihirisha kuwa zinapasuka wakati zinapokuwa zikitumika. Kasoro ni kondomu hizo kufungashwa vibaya.

Kwa hili tuna kila sababu kuwapongeza wakaguzi wa TBS kwa kuweza kubaini kuwepo kwa kondomu hizo bandarani ambazo ziliingizwa nchini kabla ya utaratibu wa kukagua bidhaa nje ya nchi haujaanza. Tunasema hivyo kwa sababu kama kondomu hizo zingechelewa kugundulika ni wazi kuwa Watanzania wengi wangezitumia wakidhani kuwa zinawasaidia kujikinga na magonjwa hasa Virusi vya UKIMWI (VVU) wakati si kweli.  Tunatoa mwito kwa Watanzania wasipuuze mwito uliotolewa na TBS kwani wao ndiyo wanatakiwa kuwa walinzi wa afya zao.

Kwa msingi huo tunatoa mwito kwa wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla kuhakikisha kondomu hizo hasambazwe kwenye soko wakati huu ambapo juhudi zinafanyika ili kuwabaini waingizaji wa kondomu hizo ili waweze kuchukuliwa hatua.

Tunasema wakati umefika sasa wa Watanzania kuondokana na kasumba ya kushabikia bidhaa mpya wakati hatuna uhakika kama zinakidhi viwango vya ubora. Ni vema Watanzania tukajenga utamaduni wa kutumia bidhaa ambazo tayari tumeishahakikishiwa ubora wake na wataalam wa TBS, kuliko zile ambazo zinaingizwa nchini tena kwa njia za panya.

Kwa hili tumeona umuhimu wa kuwepo kwa maabara ya kondomu na wataalamu waliobobea ambao wamesaidia kubaini kondomu hizo. Lakini tunatoa mwito kwa maofisa wa shirika hilo wasiishie hapo badala yake wazidi kutoa elimu kwa wananchi ili wanapoona kondomu hizo wazikatae na kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwanasa wanaohusika kuziingiza hatua itakayowezesha kuepusha madhara.

Tanzania bila bidhaa bandia inawezekana kinachotakiwa ni wadau wote kushirikiana kuzifichua kwani athari zake ni kubwa.

No comments:

Post a Comment