24 December 2012

Chipolopolo ndembendembe kwa Stars



Na Elizabeth Mayemba

TIMU ya Taifa, Taifa Stars jana wameifunga Zambia bao 1-0 katika mechi yao ya kirafiki ya Kimataifa iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mpira ulianza kwa timu zote mbili kushambuliana kwa zamu dakika ya tano Zambia walikosa bao la wazi kupitia kwa mchezaji wao James Chamanga ambaye alipiga shuti kali mpira ukagonga mwamba na kutua kwa mchezaji mwenzake Isaac Chansa ambaye naye alitaka kufunga lakini akapiga juu.

Stars dakika ya nne walikosa bao la wazi baada ya Hamisi Mcha kutoa pasi iliyomkuta SHomari Kapombe akiwa eneo la hatari alipiga mipira kwa kichwa lakini ukagonga mwamba, dakika 26 Stars walikosa bao tena baada ya Ngassa kutoa opasi kwa Kapombe lakini shuti lake lilidakwa na mlinda mlango wa Zambia Danny Munyao.

Kosakosa kwa Stars iliendelea baada ya Ngassa kufanikiwa kuwatoka mabeki wa Zambia akiwa yeye na kipa na kumdakisha, dakika 45 Ngassa aliwanyanyua mashabiki wa Tanzania baada ya kufunga bao akipokea pasi kutoka kwa  Mwinyi Kazimoto.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kushambuliana dakika 53 Zambia walikosa bao kupitia kwa James Chamanga ambaye alipiga shuti na Kaseja akaokoa, dakika ya 56 Stars walikosa bao baada ya Ngassa kuwachambua mabeki wa Zambia akiwa yeye na kipa mpira akaupiga pembeni.

Stars waliendelea kulisakama lango la Zambia dakika ya 71 mchezaji Simon Msuva aliyechukua nafasi ya Hamis Mcha alikosa bao la wazi baada ya Kazimoto kutoa pasi nzuri lakini kipa akaipangua. Mpira, dakika ya 74 Zambia walikosa bao kupitia kwa Mukuta Mulenga aliyeingia kipindi cha pili na mpira kugonga mwamba na kurudi uwanjani.

Hadi mpira unamalizika Stars 1-0, mashabiki wa Zambia ambao walikuwa kwa wingi uwanjani walitoka huku wakiwa hawaamini matokeo

Kikosi cha Stars,Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Agrey Morris, Kelvin Yondan, Frank Dumayo, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Mrisho Ngassa, Mwinyo Kazimoto na  Khamis Mcha.

Kikosi cha Zambia,Danny Munyao, Chintu Kampamba, Hichani Himonde, Chisamba Lungu,James Chamanga, Moses Phiri, Christopher Katongo, Felix Katongo, Nathan Sinkala, Roderick Kabwe na Issac Chansa.

No comments:

Post a Comment