28 December 2012

Polisi wawili mbaroni kwa mauaji


Na Mwajabu Kigaza, Kigoma

JESHI la Polisi mkoani Kigoma, linawashikilia askari wake
wawili kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mkazi wa Kijiji cha Herushingo, Tarafa ya Makere, wilayani Kasulu.


Taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari jana na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Fraisser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 25 mwaka huu, saa nne usiku katika kijiji hicho.

Aliwataja askari hao kuwa nmi D.8622 CPL Peter na G.1236 PC Sunday wa Kituo Kidogo cha Rerushingo ambao wanadaiwa kumshambulia Bw. Gasper Mussa (36) ambaye ni mkulima
katika baa waliyokuwa wanakunywa na baada ya kumpiga,
walimfikisha kituoni hapo.

Alisema siku Desemba 26 mwaka huu, Mkuu wa kituo hicho alitoa taarifa Kituo cha Polisi Kasulu kwa SP Sospeter Kunguru kuwa mtuhumiwa alikuwa mgonjwa lakini alifariki muda mchache
baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu.

“Chanzo cha ugomvi ni baada ya marehemu kushindwa kulipa vinywaji alivyokunywa ndipo askari walianza kumshambulia na
kumsababishia maumivu yaliyosababisha kifo chake,” alisema.

Alisema kutokana na tukio hilo, askari hao wamekamatwa na wanashikiliwa polisi kwa uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo hasa cha ugomvi huo na kama itabainika walihusika moja kwa moja watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia Bw. Hassan Shija, ambaye ni Mwalimu wa Chuo cha Ufundi VETA, mkoani humo, baada ya kumjeruhi mkewe kwa mapanga katika mikono yote miwili na mgongoni kutokana na wivu wa mapenzi.

Kamanda Kashai alisema, kuwa tukio hilo lillitokea Desemba 24 mwaka huu, saa nne usiku ambapo Bw. Shija ambaye ni mwalimu wa umeme chuoni hapo, alimjeruhi mkewe Bi. Rida Mbilinyi (35).

Alisema katika ytukio hilo, Bi. Mbilinyi alipata majeraha makubwa na kulazimika kulazwa kwenye Hospitali ya Mkoa Maweni kwa matibabu zaidi.

Aliongeza kuwa, hadi sasa mtuhumiwa yupo chini ya ulinzi na atafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

No comments:

Post a Comment