24 December 2012
Ni Lema tena ubunge Arusha *Ashinda rufaa iliyofunguliwa na wanachama CCM *Arusha wajipanga kumuandalia mapokezi makubwa *Dkt. Slaa, Mbowe, Lissu wazungumzia ushindi wake
Na Waandishi Wetu
MAHAKAMA ya Rufaa Dar es Salaam, jana ilitoa hukumu ya kihistoria kwa kumtangaza Bw. Godbless Lema, kuwa mbunge
halali wa Jimbo la Arusha Mjini, kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Bw. Lema alivuliwa ubunge huo na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga ushindi wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu 2010.
Wanachama hao ni Bw. Mussa Mkanga, Bi. Agness Mollel na Bi. Happy Kivuyo ambao walidai katika kampeni za uchaguzi huo,
Bw. Lema alimdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Bi.
Batilda Burian kwa kutumia lugha ya matusi.
Baada ya Mahakama Kuu kutengua ubunge huo, Bw. Lema alikata rufaa ambayo jana ilitolewa hukumu. Katika kesi hiyo wanachama hao walipinga rufaa hiyo kupitia kwa wakili wao Alute Mughwai.
Hukumu ya Bw. Lema kurudishiwa ubunge wake, ilisomwa saa 2.30 asubuhi na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo Bi. Elibeth Mkwizu mbele ya Majaji Natalia Kimaro na Salumu Massati.
Akitoa hukumu hiyo, Bi. Mkwizu alisema sababu zilizoifanya Mahakama hiyo kumrudishia Bw. Lema ubunge wake ni hoja
mbili kati ya 18 zilizowasilishwa na mawakili wake.
Kati ya hoja hizo, moja iliibuliwa na Mahakama juu ya uhalali wa wapiga kura kufungua kesi hiyo ambapo hoja ya pili, kulikuwa hakuna viambatanisho katika kesi hiyo.
Lissu nje ya Mahakama
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusomwa hukumu hiyo, Bw. Tundu Lissu ambaye ni mwanasheria wa Bw. Lema, alisema hakwenda Mahakamani kupiga ramli ambapo hukumu
hiyo imeingia katika historia.
“Kati ya wabunge 23 wa CHADEMA, 14 walishitakiwa na wapiga kura ambao hawana uwezo wa kufungua kesi pamoja na kuweka mawakili, hukumu hii inadhihirisha wazi jinsi Bw. Lema alivyoonewa ili kukidhoofisha chama,” alisema.
Aliongeza kuwa, kisheria kuna makundi ya aina nne ambayo kila moja lina mpaka wake, kundi la kwanza ni wapiga kura ambao kama walifanikiwa kupiga kura haki yao mpaka wao unaishi hapo.
Kundi la pili ni wateuliwa, kundi la tatu wagombea wenyewe na la mwisho ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo makundi hayo yana uwezo wa kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Alisema jambo la ajabu, kesi zote zilizofunguliwa dhidi ya wabunge wa CHADEMA, walalamikaji ni wapiga kura hivyo kwa hukumu hiyo, umma utakuwa umefahamu ukweli jinsi chama hicho kinavyonyimwa haki za msingi.
“Mimi mwenyewe nilishtakiwa na wapiga kura kabla ya Bw. Lema, pia Dkt. Willibrod Slaa (Katibu Mkuu CHADEMA), akiwa mbunge wa Jimbo la Karatu alishtakiwa mara tatu na wapiga kura, Mbunge wa Hai (Mwenyekiti wa chama hicho Taifa), Bw. Freeman Mbowe, naye alishtakiwa na wapiga kura,” alisema Bw. Lissu.
Dkt. Slaa azungumza
Kwa upande wake, Dkt. Slaa alisema hukumu hiyo inaonesha ni jinsi gani Mahamama ya Rufaa ilivyomuumbua Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kwa kauli yake ya kumwambia Bw. Lema mchochezi na wote wanaotumiwa na CCM kufungua kesi huku wakijua hawawezi kushinda.
Alisema CHADEMA haitawasamehe wala kuwaonea huruma madiwani wa Arusha na wengineo ambao wanatumiwa kukihujumu chama hicho na lazima walipe ghalama za kesi.
“Hadi sasa madiwani wa Arusha waliofungua kesi na kushindwa, wameshalipa nusu ya ghalama ya kesi, baada ya mwezi mmoja wanatakiwa kumalizia pesa iliyobaki na wasipofanya hivyo, watakwenda jela na kamwe hatuwaonei huruma,” alisema.
Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Mbowe, alisema wote waliopewa dhamana ya kutoa haki na kuongoza nchi hii lazima watende haki kwani ghalama iliyotumika tangu kuanza kwa kesi
ya Lema ni sh. bilioni 400 pesa ambazo zingetosha kujenga zahanati na shule lakini zimepotea kwa baadhi ya watu kutotenda haki.
“Katika mchakato wa Katiba wa Mpya, CHADEMA ingependa kuona wale wasiotenda haki, wanashughulikiwa kisheria kwa kuwajibishwa kutokana na kushindwa kutoa maamuzi sahihi.
“Wanaofikiria kuwa CHADEMA kuna mgogoro, wasahau kwani tupo imara na kazi kubwa tuliyonayo ni kuwatete wanyonge na kesi hii imechukua majaji wengi kuliko kesi zote,” alisema.
Lema azungumzia ushindi
Akizungumza na wafuasi wa chama hicho, Bw. Lema alisema mapumziko ya 'hanimuni', aliyokaa nje ya ubunge, yamempa maarifa zaidi ya kutetea haki za wanyonge baada ya mahakama
kumpa zawadi ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Lema kupokelezwa kifalme Arusha
Muda mchache baada ya Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam, kutoa hukumu ya kumrudishia Bw. Lema ubunge wake, CHADEMA mkoani Arusha kimedai kuandaa mapokezi ya kifalme kwa
mbunge wao.
Akizungumza na Majira, Katibu wa chama hicho jijini humo, Bw Amani Golugwa, alisema Bw. Lema atapokelewa kwa maandamano
maalumu ambayo yataanzia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa mkoani Kilimanjaro (KIA), hadi Arusha Mjini na kuhutubia mkutano wa ghadhara.
Alisema mbali ya mapokezi ya kifalme, Bw. Lema ataendelea kutetea wanyonge jimboni humo ambao wanaonewa na baadhi
ya watendaji wa Serikali.
Arusha furaha tupu
Katika hali isiyo ya kawaida, wanawake ambao ni wafanyabiashara wadogo jijini Arusha, jana waliacha kuuza bidhaa zao na kutanda barabarani huku wakiimba nyimbo yenye ujumbe unaosema “Baba yao mzazi yupo huru”.
Wanawake hao walisema, kitendo cha Bw. Lema kurudishiwa ubunge wake kutawafanya wapate haki zao za msingi ambazo
awali walikuwa wananyimwa kutokana na itikadi za kisiasa
zilizotanga katika jiji hilo.
“Tupo radhi leo kushangilia ushindi badala ya kuuza bidhaa zetu, tuna furaha kubwa hivyo tunachosubiri ni kumpokea Bw. Lema ambaye sisi tunaamini ndiye Rais wetu,” walisema.
Walimtaka Bw. Lema baada ya kurejea jimboni humo, atekeleze ahadi zake kwa wananchi ambazo alizitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 ambazo alishindwa kuzitekeleza kutokana na misukosuko ya kisiasa.
Viongozi CCM wateta
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa CCM jijini humo, ambao hawakutaka majina yao kuandikwa gazetini, walisema mbali ya Bw. Lema kurudishiwa ubunge wake, bado kuna umuhimu mkubwa wa wakazi wa jiji hilo kuungana na kuwa kitu kimoja.
Walisema kwa sasa kinachoitajika ni kuendeleza gurudumu la siasa zenye uhakika ambazo zitakuwa na tija katika jiji hilo na kusahau yaliyopita.
Msingi wa kesi
Bw. Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotengua ubunge wake na kuitaka imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.
Pia aliitaka mahakama hiyo iwaamuru walalamikiwa katika
shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na zile za kesi iliyomalizika kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika madai mengine, Bw. Lema anamlalamikia Jaji Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo kuwa alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi na kupuuza ushahidi uliotolewa mahakamani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
TUNACHOOMBA ARUSHA NI AMANI NA UTENGAMANO ARUSHA NI VEMA NIMKUMBUSHE LEMA KUWA SOMALIA CHINI YA GENERALI SIAD BARE KULIKUWA NA AMANI NA UTENGAMANO DEMOKRASIA BANDIA YA MATAIFA YA MAGHARIBI ILIFADHILI VYOMBO VY PROPOGANDA VIKIMTANGAZA KUWA NI DIKTETA MKAKA AKAONDOLEWA JE DEMOKRASIA IMEFIKIWA ??? MARIKANI ILIWAHI KUTOA UFADHILI MKUBWA KWA PAKSTAN IKONGOZWA NA GENERAL DIKTETA MUSHARAF ILI TU AWASAIDIE WAMSAKE OSAMA SI KWELI MARIKANI INAZINGATIA DEMOKRASIA KWAO MASLAHI KWANZA DEMOKRASIA BAADAYE NIMESHUHUDIA KWA MACHO YANGU VIDEO ILIYORUSHWA KUTOKA SOMALI TAR.20/12/2012 BINADAMU KAMA KUKU,NG'OMBE AU NGAMIA AKIELEKEZWA KIBLA HUKU DUA ZIKISOMA AKACHINJWA TUNAOMBA AMANI ARUSHA NA TANZANIA RADIO NA TELEVISHENI YA SAFINA TUNAOMBA HILI LIOMBEWE SHETANI HUYO ASHINDWE KWA JINA LA YESU IWAPO CHADEMA KUNA UFADHILI WOWOTE KATIKA KUHATARISHA AMANI YA NCHI MUNGU AUDHIBITI KAMA ALIVYOMDHIBITI MFALUME SAULI NA KUMUENZI MFALUME DAUD
ReplyDelete