27 December 2012
Nguvu zaidi inahitajika kutokomeza maralia nchini
Na Faida Muyomba
MALARIA ni ugonjwa unaoongoza kwa kuua watu wengi duniani hususani watoto walio na umri chini ya miaka mitano pamoja na kina mama wajawazito.
Takwimu za Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF), zinaonesha kuwa katika kila dakika 30, mtoto mmoja hufariki kwa ugonjwa huu duniani.
Katika Bara la Afrika pekee inaelezwa kwamba, watu milioni 350-500 huugua ugonjwa huu, ambapo wanaofariki ni watu zaidi ya milioni moja kila mwaka, hali inayoonesha kuwa unachangia kwa kiwango kikubwa kurudisha nyuma nguvu kazi ya nchi nyingi barani humo.
Nchini, watu milioni 11 wametajwa kuugua malaria, na jambo la kusikitisha, zaidi ya watu 38,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kuugua ugonjwa huu.
Kwa kulitambua tatizo hili, serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii, imeamua kuanzisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo, kwa lengo la kuokoa wananchi wake.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa na serikali dhidi ya mapambano haya ni pamoja na kugawa vyandarua vyenye viuatilifu kwa kila mwananchi kupitia kampeni yake ya 'Malaria haikubaliki’, Zinduka-Tushirikiane kuutokomeza ugonjwa wa malaria.
Katika kampeni hii iliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete, Februari 13 mwaka 2010, katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es salaam, ililenga kila mwananchi kushiriki kupambana na ugonjwa huu bila kujali dini ama itikadi za siasa.
"Kwa kila saa inayopita zaidi ya watu 10 wanakufa kwa malaria, hawa ni watu wengi mno. Kwa hiyo malaria ni janga kubwa la taifa letu lakini huu ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika," alisema wakati wa uzinduzi huo.
Wizara hiyo pia, ilisambaza vyandarua nyenye hati punguzo 4,200,000 kwa ajili ya mama wajawazito na vyandarua 1,257,020 kwa ajili ya watoto wenye umri chini ya miaka 18.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo za serikali, bado zipo changamoto kadhaa zikiwemo baadhi ya wananchi kuamua kubadilisha matumizi hayo ya vyandarua na kuvitumia kinyume na matarajio hali inayoweza kusababisha mapambano hayo kutokuwa endelevu na yenye mafanikio hapa nchini.
Mfano Wilayani Geita katika mkoa wa Geita, mkoa wa Kagera na Mwanza katika visiwa vya Ukerewe, baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia vyandarua kwa kuvulia samaki ndani ya Ziwa Viktoria, kutunzia vifaranga ili visinyakuliwe na mwewe, kwenye bustani na baadhi wakivitumia kunasa na kuhifadhia kitoweo aina ya senene ili wasioze ama kuharibika.
Kutokana na hali hii, baadhi ya watu wakiwemo wanaharakati mbalimbali, wameonesha kusikistishwa na hatua hiyo inayofanywa na baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi ikilenga kurudisha nyuma mapambano haya.
Ma’ntoga Meshack mkazi wa mjini Geita, anasema kuwa "watu wengi hawajui matumizi halisi ya vyandarua ndio maana wanavitumia isivyo, elimu ya jamii haijatolewa vya kutosha juu ya matumizi sahihi ya vyandarua, ndio maana baadhi wanatumia kuhifadhia senene kama tunavyowaona hapa mjini Geita,".
"Matumizi kama haya ya kuhifadhia senene kisha zinatumika kama kitoweo kwa wananchi, inaweza kuwa ni hatari kwa vile vyandarua hivi vina dawa aina ya Deltamethrin na Permethrin zilizotengenezwa maalumu kwa ajili ya kuua mbu waenezao malaria, lakini zinaweza kuwa na madhara kwa watumiaji wa senene ama samaki hao ambayo hatuyajui huko siku sijazo," anasema.
Anasea, baadhi ya watu wanatumia vyandarua kama mtindo kwa kuwa wana fedha za kununulia, huku wakishindwa kuharibu mazalia ya mbu kama vile madimbwi yaliyoko katika makazi ya watu na uchafu unaoweza kuwa maficho ya mbu hao.
Mkazi mwingine, Dainess Zamela, wa mtaa wa Msalala mjini Geita, anasema, "vyandarua vimetengezwa maalumu kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya malaria kwa wananchi hasa sisi kina mama wajawazito na watoto, na hivi vyandarua vimewekwa dawa hivyo kutumia kuhifadhia senene ili wasiharibike ni kuleta madhara kwa watumiaji ambayo hatuyajui.’’
John Magulu ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya afya, elimu na Mazingira katika Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, anasema elimu ndicho kikwazo pekee katika mapambano haya kwa kuwa haijatolewa ipasavyo kwa wananchi nchini juu ya matumizi sahihi ya vyandarua.
Anakiri kuwa vitendo hivyo vipo kweli na vinafanywa na baadhi yao wilayani Geita na nje ya wilaya, huku wengine wakisingizia kuwa vinatokana na umaskini jambo ambalo analipinga kuwa si kweli.
"Serikali imepoteza fedha nyingi kununua hivi vyandarua, lakini watu wachache wenye lengo la kukwamisha wanaanza kuvitumia kuhifadhia senene, kuzuia vifaranga visinyakuliwe na mwewe, lazima watendaji wote wa serikali tukiwemo sisi madiwani tuwajibike kutoa elimu kwa wananchi wetu ili kukomesha vitendo hivi,"anasema.
Ofisa uvuvi wilaya ya Geita Shafii Kitery, anasema wakati wa msako wa wavuvi haramu katika mwalo wa Makatani kata ya Nkome wilayani humo, amewahi kukamata baadhi yao wakiwa na vyandarua ambavyo walikuwa wakivitumia kuvulia samaki katika ziwa Viktoria.
"Nimeshakamata wavuvi watatu wakiwa na vyandarua ambavyo walikuwa wakivitumia kama nyavu za kuvulia samaki, hili ni kosa kubwa kwani wanasababisha kuharibu mazalia ya samaki lakini pia wanavua samaki ambao hawastahili kuvuliwa", anasema.
Mratibu wa mradi wa malaria kutoka shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia watoto la wilayani Geita(NELICO), Musa Mugaywa, anasema kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa huo nchini, yanakwamishwa na mambo mengi yakiwemo imani potofu kwa baadhi ya wananchi.
"Baadhi ya watu wana imani kuwa vyandarua vinasababisha muwasho, ugumba wengine wanadharau kuwa havina msaada kwao ndio maana hawavitumii kwa matumizi yaliyokusudiwa na badala yake wanatumia kwa kuhifadhia senene ili wasioze ama kuvulia samaki,"anasema.
Anasema, tatizo lingine linalochangia kuwepo kwa matumizi yaliyo kinyume kuwa ni kutokana na wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini, kutokuwa na vitanda vizuri na ambavyo havijakidhi mahitaji ya ukubwa wa vitanda.
"Sababu nyingine ni kuwa wananchi kwa mfano kila familia kupatiwa vyandarua vitano bure, wao wanafikiria serikali itakuwa inatoa kila mwaka, hivyo wanaona kwao ni vingi hali inayosababisha sasa wavitumie ovyo kwa shughuli kama hizi, hii yote inatokana na watanzania kutojali vitu vinavyotolewa bure", anaeleza mratibu huyu.
Akizungumzia hali hii Mratibu wa malaria wilayani Geita, Dkt.Joram Mpemba, anasema "ni makosa kwani vimetengenezwa kwa ajili ya kuua mbu waenezao malaria, hivyo matumizi haya wanayoyatumia tofauti yanaweza kusababisha madhara kwa binadamu, lakini vikitumika inavyotakiwa vinapunguza na kuzuia kwa kiwango kikubwa ugonjwa huo,".
Anasema, takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2011 kulikuwa na vifo vya watoto 135 na watu wazima 125 lakini katika kipindi cha kuanzia Februari hadi Oktoba mwaka huu, tulikuwa na wagonjwa 38,845 ambao ni watoto ambapo waliofariki ni 79 tu na watu wazima waliougua malaria walikuwa 26672 kati yao 93 ndio walifariki.
"Sasa ukiangalia utabaini kuwa vimeonesha kupungua kutokana na matumizi ya vyandarua pamoja na unyunyiziaji wa dawa aina ya ukoko majumbani,"anasema.
Anayataja madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi kwa kutumia vyandarua kuhifadhia senene kuwa, ni pamoja na matatizo kwenye figo, kuwashwa ama kukojoa mara kwa mara na endapo waliotumia senene hizo wanaweza kuwa katika hatari ya kuharisha endapo watatumia dozi kubwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Geita, Manzie Mangochie anasema, vitendo hivyo vinachangia kurudisha nyuma malengo ya serikali ya kupambana na ugonjwa huo.
"Inasikitisha, wanapaswa kufahamu kuwa ni aibu kuvitumia vyandarua kwa ajili ya senene ama kuvua samaki, serikali iliamua kuhamasisha matumizi ya vyandarua ili kuokoa maisha ya wananchi na si hayo. Hivyo nimeagiza watendaji wachukulie hatua kwa wale wote wanaoenda kinyume na tabia hii inatakiwa kuachwa mara moja," anasema.
Anawataka wananchi na wanaharakati wa masuala ya afya, kujitokeza kuwafichua watu wote wanaogeuza matumizi ya vyandarua kama yalivyokusudiwa na serikali kwa shughuli zao binafsi ili viweze kukomeshwa.
Wataalamu wa afya wanasema, mafanikio zaidi yameanza kujitokeza kwa makundi ya kina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ambao ndio wanachukua asilimia kubwa katika kuugua ugonjwa huo na hatimaye kupoteza maisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment