24 December 2012

Lake View yafaulisha wanafunzi wote VII


Na Daud Magesa, Mwanza

SHULE ya Msingi Lake View, iliyopo katika Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza, imeshika nafasi ya kwanza wilayani humo kwa kufaulisha wanafunzi wote 74 waliofanya mtihani wa darasa
la saba mwaka huu.

Ushindi huo ni wa kwanza tangu kuanzishwa Wilaya hiyo
ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Mwanza Vijijini ambapo
wavulana watano na wasichana watatu, wamechaguliwa
kujiunga na shule maalumu.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa shule hiyo, Bw. Benard Kipeja, alisema ushindi huo umetokana na walimu kujituma katika kazi pamoja na wanafunzi kuzingatia kile wanachofundishwa.

“Haya ni mafanikio makubwa na kujivunia lakini hayakuja hivi hivi bali ni juhudi za walimu katika kufundisha na ofisi ya utawala kuwa nao karibu kwa maana ya kuwasimamia ili kuhakikisha kila mwalimu anatimiza wajibu wake,” alisema.

Alisema shule hiyo inapokea wanafunzi wa aina mbalimbali wakiwemo wale ambao wazazi wao hawana uwezo ili kuwapa
fursa sawa na watoto wengine kupata elimu bora.

Wakati shule hiyo ikishika nafasi ya kwanza wilayani humo, Shule ya Msingi Alliance, imeshika nafasi ya kwanza katika Wilaya ya Nyamagana ambapo Shule ya Peace Land, imeongoza kwenye
Wilaya ya Ukerewe.

Mkoa huo ulikuwa na watahiniwa 82,419 kati yao, 56,482 wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza sawa na asilimia
68.5, ukilinganisha na asilimia 61 mwaka 2011.

Ofisa Elimu mkoani humo, Bw. Hassan Maulid, alizipongeza shule zilizofanya vizuri kwa kushika nafasi za kwanza katika Wilaya zao kutokana wanafunzi wengi kupata alama za juu.

Alisema 62 wamefutiwa matokeo kati ya 478, waliotuhumiwa kufanya udanganyifu.

No comments:

Post a Comment