24 December 2012

CUF: Tunalaani vurugu, mauaji ya raia


Na Goodluck Hongo

BARAZA Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF), limelaani matukio ya vurugu na mauaji ya raia wanayodai kusababishwa na Jeshi la Polisi nchini na kumtaka Mkuu wa jeshi hilo, IGP Said Mwema,
kuwachukulia hatua askari waliohusika.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw. Julius Mtatiro, alisema baraza hilo pia limelaani matumizi mabaya ya silaha bila kuchukua tahadhari.

“Baraza hili lilikutana Desemba 17-18, kati ya maazimio ambayo yamefikiwa ni pamoja na kulaani mauaji ya mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daud Mwangosi,” alisema Bw. Mtatiro.

Alisema kutokana na hali hiyo, CUF inamtaka IGP Mwema, kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu askari wote waliohusika kusababisha mauaji badala ya kuwalinda.

Aliongeza kuwa, chama hicho hakiungi mkono suala la wananchi kujichukulia sheria mkononi badala yake kinasisitiza utendaji wa haki kwa pande zote.

“Wajumbe wa mkutano walilaani nguvu kubwa iliyotumiwa na vyombo vya dola kukandamiza demokrasia na kukisaidia Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ili kishinde,” alisema.

Wakati huo huo, baraza hilo limemteua Bw. Hamad Masoud kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar baada ya kupata kura 39 za ndiyo na moja ya hapana dhidi ya mpinzania wake Bw. Riziki Omary Juma ambaye alijitoa katika hatua za awali kabla kura hazijapigwa.

Bw. Mtatiro alisema awali nafasi ya Katibu Mkuu Zanzibar, ilikuwa ikishikiliwa na Bw. Ismail Jussa Ladhu ambaye aliomba kupangiwa kazi zingine na chama ili aweze kuwatumikia wananchi wake wa Jimbo la Mji Mkongwe Zanzibar.

Alisema chama hicho kimemvua uanachama Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Somanga-Ndumo, wilayani Kilwa Bw.
Yusuph Amano Muhani, kwa uongozi mbaya.

“Sababu za kumvua uanachama ni uongozi mbaya kwa wananchi wake, hili ni fundisho kwa viongozi wengine wa CUF ambao utendaji kazi wao si mzuri kwani chama chetu hakipo tayari
kuwavumulia,” alisema.

Kikao cha baraza hilo ambacho kiliongozwa na Mwenyekiti wa
CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, kilijadili ajenda tano ambazo  ziliwakilishwa na Kamati ya Utendaji ya chama hicho likiwemo suala la kuimarisha chama hicho mwaka 2013.

1 comment:

  1. NI UONGO NA UNAFIKI TENA MKUBWA TU MUMECHELEWA SANA MAKANISA YAMECHOMWA KIMYA BADO MUKATETEA SHEIKH PONDA AACHIWE ,KUWEPO MJADALA WA KITAIFA KUHUSU AMANI WAKATI WAKRISTO MIUNDO MBINU WALIOJITESA KUIJENGA BILA MSAADA WA SERIKALI IKICHOMWA MOTO SINA UHAKIKA MUKISHIKA NCHI HILI SWALI HAMTAULIZWA DINI KUCHANGANYWA NA SIASA HUKO NIGERIA BOKO HARAM WANAANGAMIZA WATU NA MALI ZAO WALA HAKUNA ANAYELAANI,HUKO SOMALIA AL SHABAAB WANAANGAMIZA WATU NA MALI HAHUNA ANAYELAANI IKO VIDEO INAYOONYESHA BINADAMU WA IMANI TOFAUTI AKICHINJWA HUKO SOMALIA KAMA KUKU,NG'OMBE AU NGAMIA HAKUNA ALIYELAANI ANGEKUWA MZUNGU SOMALI INGETEKETEZWA KWA MABOMU ,MALI KASKAZINI MAUAJI NA UHARIBIFU WA MALI UNAENDELEA HAKUNA ANAYELAUMU INADHIHIRISHA HUKO MBELE UMWAGAJI DAMU WA KUTISHA UTASHUHUDIWA JUU YA USO WA DUNIA MUNGU AIREHEMU DUNIA YAKE

    ReplyDelete