17 December 2012
JK kufanyia kazi sera ya Dk. Slaa *Atafakari kupunguza kodi vifaa vya ujenzi *Azishukia halmashauri kuhusiana na ardhi
Na Goodluck Hongo
RAIS Jakaya Kikwete, amesema ataangalia uwezekano wa kushiriki mchakato wa namna ya kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi, lakini si kuifuta kabisa kwa kuwa hakuna Serikali inayoweza kuendeshwa bila kukusanya kodi.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa nyumba 290 za bei nafuu za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), zilizopo Kibada nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
"Kwa hili la gharama za vifaa vya ujenzi kuondolewa kodi kabisa haliwezekani kwani hakuna Serikali inayoendeshwa bila kodi, lakini nitajitahidi kuangalia uwezekano wa kuipunguza ingawa si kwa mwaka huu, kwani bajeti tayari imeshapangwa na hili nitalichukua,"alisema Rais Kikwete.
Alisema gharama Kwa vifaa vya ujenzi na viwanja si kwa NHC tu, bali ni watu wote. "Kama tukifuta kodi basi kutakuwa hakuna Serikali," alisisitiza Rais Kikwete.
Kauli hiyo ya Rais inaonekana kutaka kushabiiana na sera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokuwa ikitolewa na mgombea urais wake katika uchaguzi wa mwaka 2010, Dkt. Wilbroad Slaa, kuwa iwapo chama hicho kitashika dola kitafuta kodi kwenye vifaa vya ujenzi.
Hata hivyo, sera hiyo ya CHADEMA ilikuwa ikipingwa vikali na viongozi wa CCM kiasi cha kusababisha malumbano makali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu ugumu wa utekelezaji wake, huku Dkt. Slaa akisisitiza kuwa hilo linawezekana.
Hatua ya Rais Kikwete kutoa ahadi hiyo ilitokana na ombi lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, ambapo alisema kodi katika vifaa vya ujenzi inachangia kuondoa dhana nzima ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
"Ni vema na nyie NHC mkaangalia uwezekano wa kuanzisha taasisi yenu ya kifedha ili muweze kujikopesha na kuwakopesha wananchi ambao wanataka kununua nyumba hizo, kwani tatizo kubwa la wananchi si gharama bali ni jinsi ya kupata fedha hizo za kununua nyumba," alisema Rais Kikwete
Alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa NHC ni kuwapatia nyumba wananchi wa kipato cha chini, hivyo kujengwa kwa nyumba hizo kutatimiza lengo la kuanzishwa kwa NHC.
Mbali na kutoa ahadi ya kuangalia namna ya kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi, Rais Kikwete aliwashukia wanasiasa wakiwemo madiwani kwenye halmashauri kuwa wanachangia kuwaumiza wananchi kwa kugeuza ardhi kama sehemu ya vyanzo vya mapato, wakati ni huduma kama zilivyo huduma zingine.
"Halmshauri ziache kutumia ardhi kama vyanzo vya mapato, kwani haiwezekani wanunune ardhi kwa sh.milioni sita na kuiuza kwa sh.milioni 300," alisema na kusisitiza kuwa; "Hilo haliwezekani kabisa."
Alisema ni vizuri Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi kuangalia suala hilo na ifikie mahali tatizo liwe na mwisho. "Kama hayo hayatatendeka basi kuna uwezekano mkubwa wa wananchi kushindwa kumiliki ardhi kutokana tabia hii ambayo halmashauri wanaifanya,"alisema.
Alisema halmashauri kufanya hivyo hazijali maslahi ya watu wao. Alisisitiza kuwa maamuzi hayo yamekuwa yakiumiza wananchi. Aliwashukia madiwani kwa kupitisha maazimio yanayoumiza wananchi na kutolea mfano Halmashauri moja nchini.
Alipongeza NHC kwa kazi na mipango mizuri ambayo wamepanga na kwamba anaamini kuwa Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mkurugenzi Mkuu (Mchechu) itaweza kufikia malengo iliyojiwekeza kama ilani ya CCM inavyosema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment