13 December 2012

Jaji akwamisha rufaa ya Zombe


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Rufaa, Dar es Salaam, jana imeshindwa kuanza kusikiliza rufaa ya Serikali kupinga hukumu iliyompa ushindi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP) Abdallah Zombe na wenzake kutokana na mmoja kati ya Majaji waliopangwa kusikiliza kesi hiyo kuumwa.

Rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa na Majaji watatu ambao ni Semistodes Kaijage, Nathalia Kimaro na Katherine Oriyo.

Mmoja wa Majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Kimaro aliieleza mahakama hiyo kuwa, Jaji Kaijage anaumwa hivyo anaahirisha shauri hilo hadi msajili wa mahakama hiyo atakapowapa taarifa.

Mawakili wa Serikali ambao jana walikuwepo mahakamani hapo ni Vitalis Thimos, Edwin Kakolaki, Angaza Mwipopo, Prudens Rweyongeza, Muhaya Mutaki na Peter Njike.

Baadhi ya mawakili wa upande utetezi ni Richard Rweyongeza, Bw. Majula Magafu, Bw. Gaudes Ishengoma na Bw. Denis Msafiri.

Mbali ya Bw. Zombe, washtakiwa wengine waliokuwepo ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Konstebo Jane Andrew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emanuel Mabula na Koplo Felix Sedrick,

Wengine ni Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, , Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi. Ambaye hakuwepo mahalamani ni Koplo Rashid Lema (aliyefariki kabla ya kujitetea).

Washtakiwa hao wote jana walifika mahakamani hapo tayari
kwa kuanza kusikiliza shauri hili.

Bw. Zombe na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, mkoani Morogoro na dereva wa teksi, mkazi wa Manzese Dar es Salaam na waliachiwa huru Agosti 17,2009 na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Wafanyabiashara waliouawa ni Sabinus Chigumbi maarufu 'Jongo', Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, ambaye ndiye alikuwa dereva teksi. Bw. Zombe na wenzake walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao wanarejea tena mahakamani, ikiwa imepita miaka tatu na miezi mitatu tangu waachiwe huru kutokana na hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati.

Katika hukumu yake, Jaji Massati alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao bila kuacha mashaka.

Alisema mahaka ilibaini wauaji halisi hawajafikishwa mahakamani hivyo mashtaka dhidi ya washtakwa waliokuwapo mahakamani hayawezi kutengenezeka na kuiagiza Jamhuri kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wauaji halisi.

Hoja za Serikali katika rufaa hiyo namba 254/2009, iliyofunguliwa Oktoba 6, 2009, imebainisha sababu 11 ambazo zimeifanya ipinge hukumu hiyo na kudai kuwa, kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote walikuwa na hatia.

Katika hoja hizo, Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ilibainisha kuwa kulikuwa na upungufu katika hukumu hiyo kwa kila mshtakiwa.

DPP anadai kuwa, Jaji Massati alipotoka na kushindwa kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu mashtaka ya jinai na kwamba alijichanganya sana katika hukumu hiyo.

Alidai kumshangaa Jaji Massati kwa kushindwa kuwatia hatia washtakiwa wote licha ya kwamba kulikuwa na ushahidi wa
dhahiri na kimazingira ambao ulitosha kuwatia hatiani.

Idadi kubwa ya watu walikuwepo mahakamani hapo ili kuangalia majibizano ya hoja kwa mawakili wa Serikali na washtakiwa.

No comments:

Post a Comment