28 December 2012

Hali ya Padri Mkenda sasa yaimarika


Na Goodluck Hongo

HALI ya Papri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar, Ambrose Mkenda (55), aliyejeruhiwa kwa risasi juzi na watu wasiofahamika nje ya nyumba yake wakati akitoka katika Ibada ya Krismasi, hivi sasa inaendelea vizuri.


Padri Mkenda alihamishiwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi baada ya kupatwa na tukio hilo na kulazwa katika Chumba cha
Watu wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika Taasisi ya
Tiba ya Mifupa (MOI), lakini jana alihamishiwa wodini.

Wakati hali ya Padri Mkenda ikiendelea vizuri, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Abood, imesema itahakikisha inafanya uchunguzi
ili wa kina kubaini chazo cha tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada
ya kumjulia hali Padri Mkenda, Bw. Abood alisema Jeshi la Polisi Zanzibar linaendelea kuwasaka kwa nguvu watu waliohusika na tukio ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Wananchi wasiwe na wasiwasi, Jeshi la Polisi Zanzibar linafanya uchunguzi wa kina kuwabaini wahusika na chazo cha tukio hili la kusikitisha na mengine yaliyowahi kutokea,” alisema Bw. Abood.

Aliongeza kuwa, jeshi hilo linafanya kazi usiku na mchana ili kupambana na wahalifu hivyo wananchi wasiwe na hofu kwani wahusika lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Akizungumzia hali ya Padri Mkenda, Ofisa Habari wa Kitengo
cha Mifupa MOI, Bw. Alams Jumaa, alisema afya ya Padri huyo
inaendelea kuimarika ambapo hivi sasa anaweza kuongea na
kujitambua tofauti na alivyokuja.

Alisema Padri Mkenda alipata majeraha kwenye kidevu lakini hajatolewa jino hata moja. Padri huyo alipigwa risasi shavuni wakati akitoka kanisani kwenda katika Hosteli ya Tomondo anayoishi na watumishi wengine wa kanisa hilo.

No comments:

Post a Comment