24 December 2012
Dkt. Huvisa azidi kuonesha makali yake *Aagiza Meneja Hoteli ya Jangwani akamatwe
Na David John
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Terezya Huvisa, ameliagiza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), kumkamata Meneja wa Hotel ya Jangwani Resort ya Dar es salaam.
Pia Dkt. Huvisa ameagiza kukamatwa Msimamizi wa ujenzi unaoendelea hotelini hapo Bw. Abdraman Natal, kwa kukaidi maagizo yalitolewa na viongozi wa baraza hilo kuhusu
kuboresha mazingira ya hoteli.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam jana, Dkt. Huvisa alisema moto aliouwasha hauzimiki hadi wamiliki wa hoteli zote nchini watakapotekeleza maagizo wanayopewa ili kutekeleza sera za uhifadhi wa mazingira kwa vitendo.
Alisema katika kuhakikisha sheria ya mazingira namba 20 ya
mwaka 2004 inalindwa, wameifungia hoteli hiyo na kutoa
maagizo mazito baada ya uongozi wa hoteli hiyo kukaidi
maagizo waliyopewa ya kuboresha mazingira.
“Nimeagiza NEMC ihakikishe inawachukulia hatua zinazostahili wamiliki wote wa hoteli ambao wameshindwa kutekeleza maagizo ya kukarabati hoteli zao,” alisema.
Dkt. Huvisa aliongeza kuwa, hoteli nyingi zinakabiliwa na tatizo la kutokuwa na mifumo mizuri ya kupitisha maji taka na kuweka fukwe katika hali ya usafi hivyo kuhatarisha usalama wa wateja
hasa ukizingatia kuwa, hoteli hizo zinapokea watu wa kila aina kutoka nje na ndani ya nchi.
Alisema atahakikisha anazifungia hoteli zote ambazo hazitazingatia masherti wanayopewa hasa kuhusu uhifadhi wa mazingira.
Katika hatua nyingine, Dkt. Huvisa alisema amemwandikia ripoti Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal ya kuwashtaki viongozi wa Jiji la Dar es salaam na Halmashauri ya Kinondoni kwa kushindwa kuitikia wito wa kikao chake kilichozungumzia hali ya uchafu ambao umekithiri katika jiji hilo.
Alisema ingekuwa ni amri yake, angechukua sheria stahiki kuhusu viongozi hao kwa kushindwa kusimamia suala hilo hivyo ameamua kulipeleka kwa Dkt. Bilal na nakaya yake kumpa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kwa maamuzi zaidi.
Pia Dkt. Huvisa alizungumzia tatizo la uharibifu wa mazingira linavyoikumba dunia ambapo Novemba 27 hadi Desemba 7 mwaka huu, walikuwa na Mkutano wa 18 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Mjini Doha Qatar.
Alisema lengo la mkutano huo lilikuwa kujadili kuhusu kuanza kwa awamu ya pili ya utekelezaji wa mkataba au itifaki ya kyoto na urefu wa kipindi cha utekelezaji wake.
Mambo mengine yaliyojadiliwa ni viwango vya upunguzaji gesi joto kwa nchi zilizoendelea wakati wa utekelezaji, upatikanaji fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kuwezesha Mfuko wa Mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kikao hicho pia kilijadili upatikanaji na utoaji fedha ili kuzuia uharibifu wa misiti, jinsi ya kukabiliana na upotevu, uharibifu wa mali na maisha ya watu kutokana na athari za mabadiliko hayo pamoja na matumizi ya sekta ya kilimo kukabiliana na mabadiliko hayo.
Alisisitiza kuwa, ofisi yake ipo kwa ajili ya kusimamia sheria zilizowekwa si vinginevyo hivyo atahakikisha anatekeleza hilo kwa wote ambao watakaidi kufuata maagizo yanayotolewa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment