28 December 2012

CUF wambana Muhongo sakata la umeme nchini



Na Darlin Said

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimetoa wito kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuwaeleza
ukweli Watanzania kuhusu hali ya umeme nchini.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu Bw. Abdul Kambaya, ilisema umefika wakati wa Watanzania kujua
ukweli badala ya kuendelea kudanganywa kuwa tatizo la
kukatika umeme linatokana na uchakavu wa miundombonu.

Alisema kauli zinazotolewa na Prof. Muhongo kuhusu hali ya umeme nchini ni kutetea mgawo unaoendelea Dar es Salaam na
kuongeza kuwa, sekta ya umeme nchini ipo katika hali mbaya
kutokana na kukatika mara kwa mara hasa jijini humo.

Aliongeza kuwa, hali hiyo inachangia wazalishaji viwandani kukodi majenereta hali ambayo inawaongezea gharama kubwa za uzalishaji hivyo kusababisha bidhaa kupanda.

“Kama hali hii inatokana na uchakavu wa miundombinu kwanini TANESCO wasilishughulikie maana hadi sasa ni zaidi ya miezi
sita tatizo hili linaendelea,” alisema Bw. Kambaya.

Alisema kinachofanywa na serikali ni danganya toto kwa wananchi ambayo haipaswi kuendelea bali TANESCO inatakiwa kutatua tatizo na kutoona aibu kufuta kauli ya Serikali kwamba hakutakuwa na mgawo wa umeme.

Juzi Prof. Muhongo akiwa mjini Musoma, mkoani Mara, alikutana na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kudai kukatika kwa umeme mara kwa mara kunatokana na uchakavu wa miundombinu.

No comments:

Post a Comment