13 December 2012

CHILUNGO: Mwanahabari aliyepoteza mboni za macho yake


Na Rashid Mkwinda


"KINACHOTOKEA katika hisia zangu kwa sasa ni vile ambavyo niliviona zamani, vimebaki kuwa taswira ya kudumu isiyopotea…ni picha pekee iliyobaki kichwani mwangu inakuja kama sinema, hisia zangu zinatafsiri rangi na mandhari tofauti ambazo niliziona kabla sijapofuka macho yangu," anaanza kusimulia mkasa huu Mussa Chilungo(60).


Chilungo ni mwandishi wa habari ambaye kwa sasa amepoteza mboni na nuru ya macho yake, haoni chochote kinachopita mbele yake, bali kilichobaki ni hisia za sauti na kumbukumbu zinazovinjari kichwani mwake  ambazo hutumia kuzitafsiri katika fikra zake kulingana na baadhi ya milango ya fahamu aliyobaki nayo.

Milango pekee ya fahamu anayoitumia Mzee Chilungo kwa sasa ni, mdomo, pua,masikio na ngozi yake ilhali mlango mmoja wa fahamu ambao ni macho kwa sasa hayana tena uwezo wa kuona na huo ndio umekuwa ulemavu wake kwa sasa, awali alikuwa mzima mwenye macho mawili kama walivyo binadamu wengine.

Kwa mtu aliyemfahamu Mzee Chilungo awali atabaini namna alivyokuwa mahiri na mbunifu katika taaluma yake ya habari hususani katika kituo cha Redio alichokuwa akifanyia kazi cha Redio ya Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa iliyopo mkoani Lindi.

Unapokutana na Mzee Chilungo kitu cha kwanza utakachokibaini kwake ni uwezo wake wa kutambua sauti za watu aliofanya nao kazi kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini iwe kwenye taaluma ya habari ama katika utumishi wake serikalini.

Humjua mtu mmoja kwa majina ilimradi asikie sauti yake mara moja na hicho ndicho kipaji pekee cha utambuzi ambacho Mwenyezi Mungu amempatia baada ya kuondokewa na nuru  ya macho yake.

Kumbukumbu ya Mzee Chilungo inavinjari katika mawazo yake na kutengeneza taswira katika ubongo wake na hivyo kutanabahi kuwa anayeongea naye ni nani, huwezi kutofautisha uwezo wake na mtu mwingine mwenye viungo kamili, na hili ni miongoni mwa mambo ambayo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwezo wake.

"Haya ndiyo majaaliwa yangu, simlaumu Mwenyezi Mungu kunijaalia ulemavu huu, naamini kuwa kabla hujafa hujaumbika na Mungu haachi kuumba kila siku’’anasema Mzee Chilungo akielezea utukufu wa Mwenyezi Mungu na majaaliwa aliyonayo.

"Njia nilizopita zamani ninaweza kupita mwenyewe bila kuongozwa na mtu yoyote, ulemavu wangu haunizuii kufanya shughuli zangu za kila siku ijapokuwa kuna ugumu naupata lakini kwa kipindi hiki cha miaka mitatu tangu nipofuke macho yangu nimeanza kuzoea,"anasema.

Kama yalivyo mahitaji ya watu wengine wasio na ulemavu wa aina yoyote, Mzee Chilungo ana mahitaji yanayoshabihiana na watu wa aina hiyo bali kutokana na masahibu yaliyomkuta amelazimika kuikubali hali hiyo ingawa ni kwa shingo upande lakini ndio hali halisi na ndio maisha yake yalivyo kwa sasa hadi mwisho wa uhai wake.

"Ama kweli kabla hujafa hujaumbika, mie nilikuwa mzima naangalia kwa macho mawili kama ambavyo unaangalia wewe sasa hivi sina macho, natafsiri sauti kwa hisia", anaelezea kwa masikitiko Mzee Chilungo.

Mzee Chilungo ambaye ni baba wa familia ya watoto watano alizaliwa mwaka 1953 katika kijiji cha Ndekenyela wilayani Ruangwa mkoani Lindi alijipatia elimu yake ya msingi ya Kati na sekondari kati ya mwaka 1969 hadi mwaka 1972 katika shule ya Lindi sekondari ambapo kabla ya hapo akiwa shuleni mwaka 1970.

Anasema kuwa  alikuwa  ni miongoni mwa walimu waliochaguliwa kufundisha elimu ya watu wazima Lindi mjini kati ya mwaka 1973 na baadaye shule ya Jumuiya ya Wazazi iliyopo Amana Jijini Dar es salaam na baadaye mwaka 1976 alihamia mkoani Mwanza katika wilaya ya Ukerewe.

"Huko nilifundisha katika shule ya Mulutunglu na baadaye nikarejea  mkoani Lindi na kuchanguliwa kuwa Mwalimu mkuu katika shule ya msingi ya Nyangamala nafasi ambayo nilikuwa nayo kwa nyakati tofauti katika shule tofauti hadi mwaka 2000 nilipoteuliwa kuwa Ofisa Habari wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa", anasema.

Chilungo ambaye pia ni mume wa mke mmoja aliyemtambulisha kwa jina la Zainab Liwikila anasema kuwa taaluma ya habari alienda kuisomea mjini Bagamoyo ambapo baadaye aliendelea na kazi ya uandishi wa habari hadi mwaka 2009 alipopofuka macho yake.

CHANZO CHA UPOFU

Bw. Chilungo anasema kuwa hajui chanzo na tatizo halisi la ugonjwa wake bali bali anachofahamu ni kwamba alianza kupoteza nuru ya macho yake baada ya kichwa kumuuma,

"Mwanzoni nilianza kuona giza macho yalipoteza nguvu, nilienda Hospitali ya CCBRT Dar es salaam, nilielezwa kuwa nina matatizo ya shinikio la damu na macho nikapata matibabu lakini sikuweza kupata nafuu," anasema Chilungo.

Anasema kuwa fikra zake zinamuonesha picha mbalimbali kama sinema vikiwa na rangi tofauti ambavyo aliwahi kuviona kabla hajapofuka macho na kwamba hata pamoja na kuwa katika hali hiyo aliendelea na kazi hadi alipostaafu kazi ya ualimu mwaka 2011.

Amemudu kujenga nyumba baada ya kupofuka macho ilhali wakati akiwa mzima hakuwahi kuwa na uwezo wa kujenga na kwamba hilo limempa faraja kwani kwa hali aliyonayo ya upofu katika nyumba za kupanga angezidi kuwa tegemezi katika jamii.

Kuhusu kazi zake za kihabari na ushirikiano wake kwa jamii ya Wanahabari wa mkoa wa Lindi, ni Mjumbe wa kamati ya Utendaji ya Klabu anasema kuwa pamoja na kuwa katika hali hiyo ya ulemavu wa macho bado anapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanahabari wenzie wa Klabu ya Waandishi wa habari wa mkoa wa Lindi na wale wa mikoa ya nyanda za juu kusini.

"Nawashukuru wanahabari wote wa mikoa ya kusini na nyanda za juu ambao kwa moyo wao waliguswa na hali yangu tulipokutana waandishi zaidi ya 150 mkoani Iringa, wengi walitokwa na machozi na kunichangia, umoja huu uendelezwe hata kwa wengine wenye matatizo kama yangu,"anasema.

Anasema kuwa viongozi wake wa Klabu akiwemo Mwenyekiti Abdulaziz Ahmed wamekuwa wakimshirikisha katika shughuli na semina mbalimbali zinazopitia katika klabu bila kujali hali yake.

Anabainisha kuwa wapo wanahabari wenzake wanaompa ushirikiano kama vile Juma Mweru ambaye anamsaidia kuhariri na kwenda mitaani kurekodi vipindi mbalimbali ambavyo huvirusha redioni.

"Mapunda na Mweru wamekuwa ni msaada mkubwa kwangu katika hali yangu ya upofu, wananipa msaada wa kikazi na kuniwezesha nimudu vyema kazi zangu za kila siku," anasema.

Anatoa wito kwa watu wengine wenye ulemavu, kuikubali hali waliyonayo na kuishi kama zamani na kwamba matatizo ya aina hiyo yasiwe ndio mwanzo wa kuanza kuishi kwa utegemezi ambapo pia serikali na taasisi binafsi kutowatenga walemavu na kuwapa kipaumbele.


No comments:

Post a Comment