17 December 2012

Camfed yasisitiza elimu bora kwa mtoto wa kike

Na Mariam Mziwanda

SHIRIKA lisilo la kiserikali la kampeni ya elimu kwa mtoto wa kike CAMFED limeeleza haja iliyopo kuondoa matabaka kwa kueneza sera ya jinsia kwa kutoa fursa ya elimu bora kwa mtoto wa kike ili aweze kutambua haki zake za msingi.

Akizungumza na majira jijini Dar es salaam  Mwenyekiti wa bodi wa Camfed Bi Stella Bendera  alisema kuwa mpaka sasa shirika hilo limefanikiwa kunufaisha wasichana 6332 kwa ufadhili wa shule za Sekondari,wasichana na wavulana 64227 pia wamenufaika na mfuko wa SNF sambamba na wasichana 75 wa kidato cha tano na sita.

Alisema Shirika hilo ambalo limeanza mwaka 2006 likiwa limetokana na mpango wa Serikali katika utekelezaji wa mradi wa kusomesha watoto wa kike baada ya mpango huo kusitishwa Camfed iliona haja ya kuendelea kumpa nafasi mtoto wa kike aliyekosa fursa hasa kutokana na maisha magumu aliyonayo.


"Dira ya shirika hili ni kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ,analindwa na anathaminiwa huku likimuondoa katika hali ya umaskini ambapo kupitia dira hiyo Camfed imeweka dhima ya kuongeza idadi ya wasichana wanaopata elimu,kukuza na kulinda haki zao na kuhakikisha wanakua huru kutoka katika aina zote za ukandamizaji hali ambayo itapelekea uwepo wa taifa lisilo na matabaka nchini"alisema
.
Alisema CAMFED inafanya kazi katika nchi tano za Afrika ikiwemo Zimbabwe,Tanzania,Ghana,Zambia na Malawi lengo kuu likiwa ni kupunguza umaskini kwa kuwezesha elimu ya watoto wa kike wanaotoka katika mazingira hatarishi na yatima waliopo mashuleni na kuwawezesha kiuchumi wasichana wa vijijini.

Ameeleza pia mikakati ya shirika ni kuhakikisha wasichana vijana wanaotoka mashuleni wanajengewa mazingira mazuri ya kiuchumi na kuwa mfano mzuri kwa jamii zao ili kuleta mabadiliko katika taifa na familia zao.

Aidha Camfed inafanya kazi katika wilaya kumi nchini ambazo ni Kibaha,Kilolo,Iringa vijijini,Rufiji,Bagamoyo,Morogoro Vijijini,Kilombero,Pangani na Handeni na jumla ya shule 193 za sekondari na shule 351 za msingi zimepata msaada kupitia mradi wake wa ada za shule na mahitaji ya mtoto(Bursary Program) huku mfuko wa tahadhari(safety net fund) ukiwa unawawezesha watoto wa ngazi zote mahitaji ya lazima.

Wasichana wengine 58 wamepata ufadhili wa chuo kikuu ambapo kumi kati yao wamehitimu stashahada ya kwanza mwaka huu huku wasichana 1541 walioko vijijini wamenufaika na kupatiwa mitaji na mikopo ambayo imewezesha kuanzisha bishara ndogondogo ambazo kwa kiasi kubwa zimebadili maisha yao.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji CAMFED Tanzania Msaada Daudi Balula amesema katika mwaka huu wameweza kusomesha wasichana 3326 kwa kuwalipia ada huku wanafunzi zaidi ya elfu kumi wakiwa wamenufaika na mfuko wa dharula na wajumbe 117 kati ya 189 wa camfed wilaya wamepata mafunzo ya uhamasishaji  jamii na msaada wa kisaikolojia kwa watoo wanaoishi mazingira magumu.

Pia ameeleza kuwa vikundi 30 vya wazazi vimeweza kuundwa ili kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa watoto hao huku wajumbe wa Camfed na Cama wakiwa wamafanikiwa kuudhuria mafunzo nchini Zimbabwe na GHana ili kubadilishana uzoefu.

Amesema jitihada hizo za elimu bora kwa mtoto wa kike zimekwenda sambamba na uwezeshaji wa elimu ya afya  ambapo kupitia wajumbe 26 wa Cama waliopatiwa mafunzo ya ukufunzi wa afya wameweza kuelimisha jamii.

No comments:

Post a Comment