20 December 2012

Abiria 300 kivuko cha Summar III wasota saa 2



Na Daud Magesa, Mwanza

ABIRIA zaidi ya 300 waliokuwa wakitumia Kivuko cha MV Summar III, jana wamelazimika kusota kwa zaidi ya masaa
mawili baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA),
Kanda ya Ziwa, kuzuia kivuko hicho kisisafirishe abiria
ndani ya Ziwa Victoria.


TPA pia imeutaka uongozi wa kivuko hicho, kukiondoa kando
ya Bandari ya Mwanza Kaskazini ili kupisha njia ya reli.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugezi wa kivuko
hicho, Bw. Salum Ally, alidai kushangazwa na hatua hiyo ya TPA kumtaka akiondoe kivuko hicho kwenye geti waanalotia nanga na kukiingiza ndani ya Bandari ya Kaskazini, eneo ambalo si salama kutokana na kina kifupi cha maji.

Alisema TPA ilimwandikia barua Desemba 11 mwaka huu, yenye namba MN/2/3/42 ikimpa wiki tatu awe amehamisha kivuko hicho kutoka mahali kilipo, kukiingiza ndani ya Bandari ya Kaskazini na kuendelea kutoa huduma ya usafirishaji abiria.

“Baada ya kupokea barua yao, tulishauriana kipindi ambacho treni haijaanza kuingia bandarini, tuendelee na huduma lakini ghafla wamenipa barua nyingine iliyosainiwa na Kaimu Meneja wa TPA, ikiagiza nisitishe huduma mara moja,” alisema Bw. Ally.

Aliongeza kuwa, kusitishwa kwa huduma ya kusafirisha abiria imewaathiri sana wananchi wanaotegemea huduma ya usafiri
huo, kusafirsha mizigo yao ambapo wazee wasiojiweza,
wajawazito na wanafunzi huwa hawatozwi nauli.

Bw. Ally alisema eneo aliloelekezwa na TPA kwa ajili ya utoaji huduma ya usafirshaji, halifai kutokana na kina kifupi cha maji, ufinyu wa eneo husika na ukosefu wa miundombinu ya barabara
kwa ajili ya kupitisha magari ya abiria na mizigo.

“Kimsingi siwezi kupingana na Serikali wala kuondoa kivuko mahali kilipo bila maandalizi ya kutosha, ikiwezekana nitatafuta shughuli nyingine.

“Kabla ya kuchukua hatua tutashauriana na mwanasheria wangu, maana tulikuwa na mkataba na TPA, uliopaswa kumalizika Septemba 2013,” alisema Bw. Ally.

Nahodha wa kivuko hicho, Bw. Yona Ikomeja, alisema hawezi kuhatarisha abiria na chombo chenyewe kutokana na ufinyu
wa eneo hilo kutumiwa na meli MV Clarias.

“MV Summar ina upana wa futi nane, meli ya MV Clarias ina futi 16 ambazo kitaalamu si sahihi kutokana na ufinyu wa eneo, hivyo kutuma eneo tuliloambiwa tuhamie ni kuhatarisha chombo na
abiria wakati wa kutoka au kuingia pia kuna kina kifupi cha
maji,” alisema Bw. Ikomeja.

Alishauri TPA kuchimba eneo hilo ili kuongeza kina cha maji, kupanua gati na kuwataka watazame upya uamuzi huo kwani
wananchi wananyimwa haki ya msingi ya kupata usafiri.

Juhudi za gazeti hili kumpata Kaimu Meneja wa TPA, Kanda ya Ziwa, ziligonga mwamba baada ya walinzi kumzuia mwandishi asingie ofisini kwake.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Uchukuzi Dkt. Charles Tizeba, akiwa jijini Mwanza, aliiagiza TPA kuvunja mkataba na mmiliki kivuko hicho kwa madai ya kuziba njia ya reli inayoingia ndani
ya bandari hiyo kupakua nishati ya mafuta kwa ajili ya meli za kampuni ya MSC.


No comments:

Post a Comment