26 November 2012

Ziko wapi benki zitazowakomboa maskini?


Na Michael Sarungi

NI lini tutakuwa na benki zitakazoungana na  taasisi nyingine za fedha kwa ajili ya kupambana na umaskini unaowatesa Watanzania kwa muda mrefu?

Imenilazimu kuanza na swali kama hili, baada ya kufanya utafiti kwenye benki nyingi tulizonazo na kugundua kuwa asilimia kubwa ya benki zimejaa mfumo wa kibepari.

Nasema hivyo kwa sababu ni benki zinazotaka mteja wake awe na kitu ndipo aongezewe kwa alichokuwa nacho, huku wafanyakazi wake muda wote wakiwa  mezani wakisubiri wateja waende kuweka pesa au kuongelea habari za mikopo.

Nyingi ya benki hizi ambazo zimerundikana mijini, ni benki ambazo kwanza hazina urafiki wa karibu na watu maskini na nyingi zipo kwa malengo ya kuangalia faida zaidi na si kuwakomboa watu wa jamii hiyo.

Hii ni kutokana na kwamba mara nyingi benki hizi huwa zinakuwa na masharti magumu kwa mwananchi wa kawaida wakati anapotaka kuomba mkopo,kwani mara nyingi huwa zinahitaji dhamana kama nyumba zenye hati na thamani yake iwe mara mbili au tatu ya thamani ya mkopo unaohitajika.

Katika mfumo kama huu siyo rahisi kwa benki hizi tulizonazo kuwa na utamaduni wa kuwafuata wateja  walipo ili kufahamu mahitaji yao na kuwasaidia.

Benki nyingi tulizonazo hapa nchini ni zile za kumsaidia aliyenacho azidi kuneemeka na asiyenacho abaki kuzama kwenye lindi la umaskini.

Kwa maana nyingine ni ndoto za alinacha katika mifumo kama hii ya benki tulizonazo kuwa mkombozi wa kweli kwa mwananchi maskini ambaye bado anaishi kwenye nyumba ya tembe huko Kigoma

Ukifanya tathmini ya haraka utagundua kuwa Jiji kama la Dar es salaam pekee lina utitiri wa benki zaidi ya 30 achilia mbali taasisi nyingine za kifedha.

Je! ni kweli beki hizi zinatimiza malengo ya kupambana na adui umaskini kwa Watanzania walio wengi?.Na kama jibu ni ndiyo mbona hazifiki  huko walipo Watanzania wengi ambako ni vijijini?

Kwani mpaka hivi sasa hakuna hata benki moja ya kigeni au ya nyumbani inayofanya kazi zake maeneo ya vijijini kwa sababu malengo yao si ya kuwasaidia Watanzania wa hali za chini bali ni kutengeneza faida kubwa kwa kufanyabiashara na kampuni kubwa za mijini.

Na hii ndiyo maana uendeshaji wa benki hizi  zimejaa  mifumo ya kuangalia faida zaidi kuliko hali halisi ya wakazi maskini wa nchi husika hata kidogo.

Kwa mfano takwimu zinaonesha kuwa kabla ya janga hili la soko huria wateja waliokuwa na akaunti za akiba ambao wengi wao walikuwa ni wa hali ya chini walikuwa wanalipwa riba kati ya asilimia 5 mpaka 9 kwa mwaka.

Hebu angalia sasa si kuwa riba hizo zimepunguzwa kwa kiwango kikubwa mpaka kufikia asilimia 0.5 hadi asilimia 3 kulingana na salio na hapo hapo mteja anatozwa kiasi  cha pesa kwa ajili ya malipo ya huduma  (service charge).

Kwa maana nyingine ni kuwa endapo akaunti hiyo itakaa kwa muda bila ya kuongezewa pesa mteja anaweza kujikuta hana pesa yoyote au akaunti imefungwa kabisa na kulazimu kukumbana na usumbufu mwingine.

Mbali na hilo au anaweza kukuta deni kwenye akaunti yake ilhali hakuna huduma yoyote iliyotolewa  kwa mteja wa akaunti husika, je! kwa mtindo  huo kuna nia ya kuwakomboa wanyonge?

Kwa  hali hiyo  ni ukweli ulio wazi kuwa nyingi ya benki tulizo nazo ni benki zinazofanya kazi na matabaka ya watu wenye hali ya juu na kuwabagua maskini.

Hiyo inaweza kuwa ni moja ya sababu kubwa inazochangia umaskini kuzidi kutamalaki miongoni mwa Watanzania walio wengi hapa nchini.

Sababu nyingine inayochangia benki hizi  kutokujihusisha kufanya biashara na matabaka ya watu wa chini ni kuwa benki hizi zinajihusisha na biashara kubwa kubwa kwa hiyo ni riski kwao kujitumbukiza kwenye biashara ndogo ndogo.

Misimamo hiyo ya benki  zilizonyingi  hapa nchini umekuwa ni mgumu sana kwa wananchi wa kawaida kuweza kuja mijini na kujaribu kutafuta mikopo kwa malengo ya kujianzishia miradi mbali mbali.

Kwa kuufahamu ugumu na usumbufu wanaokutana nao wananchi wa hali ya chini inapofikia suala la kuomba mikopo kwenye taasisi hizi mwaka wa fedha wa 2006/07 serikali ilitoa ofa kwa baadhi ya nyumba kwenye maeneo ambayo hayakupimwa lakini bado haikusaidia.

Kwa maana hiyo njia pekee itakayoweza kuwasaidia watanzania wa hali ya chini ni kupatikana kwa benki  zitakazokuwa na nia ya dhati kuwafikia watanzania wa hali ya chini na kuangalia njia sahihi ya kuwakomboa kiuchumi kwa kuwapa mikopo ya mashariti nafuu.

Waanzilishi wa benki hizo lazima ziwe wenye mioyo ya kiuzalendo na wenye dhamira ya dhati ya kuwakomboa Watanzania maskini na si vinginevyo.

Ukiagalia kwa umakini hali halisi ilivyo sasa kwa hapa nyumbani, benki zetu wenyewe ni muhimu sana kuliko wakati wowote ukizingatia kuwa mpaka hivi sasa ni Watanzania wachache toka vijijini wenye ujasiri kwenda mijini na kufanikiwa kupewa mikopo na benki hizi za kigeni

Hapa panatakiwa viongozi wenye mioyo ya kujitolea wakiwa na nia thabiti ya kuwakomboa Watanzania wa hali ya chini kama walivyo pata kufanya akina Profesa Yunus Mohamed na wenzake toka nchini Bangladesh.

Akiwa hapa nchini karibia miaka ipatayo mitano iliyopita Profesa huyo alimweleza Rais Kikwete jinsi ubunifu wao ulivyoweza kuwasaidia wananchi wa hali ya chini kwa kiwango kikubwa nchini kwake.

Akatolea mfano kuwa moja ya mafanikio yao makubwa yalitokana na benki yao waliyoanzisha na kufanikiwa kuwawezesha omba omba wapatao 900 kuweza kuwa wajasriamali.

Ukosefu huu wa watu wenye uwezo wa kubuni miradi kama alivyofanya Prof Mohamed na wenzake limekuwa ni tatizo kwa nchi yetu, na hii ni kwa sababu wengi wa watawala wetu wanahisa kwenye benki hizi za  kigeni.

Hili ni tatizo kubwa kijamii kwani katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia pengo kati ya aliye nacho na asiye nacho kikizidi kukua kwa kasi ya ajabu.

Na wala hakuna hata juhudi za dhati za kimakusudi za kuweza kupambana na hali hii hatarishi kwa maendeleo ya Tanzania ya leo na kizazi kijacho kwa hali ya kawaida hili nalo ni bomu lingine ambalo ipo siku litakuja kulipuka.

Kibaya zaidi hata kwenye hayo benki ambako serikali ina hisa kidogo ukiritimba huo wa watu wa hali ya chini kuweza kupata mikopo kwa kiasi fulani unaambatana na ufisadi wa kutisha.

Kwa mfano kuna tuhuma kuwa viongozi wengi waandamizi wamekuwa wakichukua mikopo bila hata ya masharti tofauti  na wananchi wa kawaida anavyoweza kupewa mkopo.

Ili kuweza kuwakomboa Watanzania maskini changamoto kubwa bado inawakabili wachumi wetu na viongozi wa serikali kuweza kufanya mabadiliko ya kiuchumi kwa kuwawezesha wananchi kuinuka kiuchumi.

Na mwisho nimalizie kuwakumbusha viongozi wetu kuwa umaskini ni hali duni ya kimaisha na ambayo huenda ikakiathiri kizazi hadi kizazi na hasa panapo kosekana jitihada za makusudi  ili  kuweza kuukata myororo huo.

Kwa hiyo dawa pekee ya kuweza kuwakomboa  Watanzania ni kuachana na benki hizi zenye mfumo ya kiubepari na kuanzisha benki kama walivyofanya Profesa Mohamed na wenzake nchini Bangladesh  kwa kuanzisha benki rafiki wa maskini.



No comments:

Post a Comment