26 November 2012
Wekeni kipaumbele fani ustawi wa jamii-Meya
Na Florah Temba,
Moshi.
SERIKALI imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuweka kipaumbele zaidi kwenye fani ya ustawi wa jamii, hatua ambayo itasaidia kupunguza matatizo yaliyopo katika jamii ikiwemo vitendo vya ukatili dhidi ya
watoto na wanawake.
Ushauri huo ulitolewa na mstahiki meya wa manispaa ya Moshi, Bw. Jafary Michael wakati akifungua mkutano wa chama cha maofisa ustawi wa jamii
Tanzania (TASWO)tawi la Kilimanjaro, ambapo alisema fani ya ustawi wa jamii imesahaulika hali ambayo inawafanya wataalamu wengi wa fani hiyo
kuikimbia.
Bw. Michael alisema maofisa ustawi wa jamii wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, licha ya kuwa na jukumu nzito la kufuatilia
matatizo mbalimbali yaliyoko katika jamii ikiwemo ya ubakaji wa watoto,utelekezaji watoto na hata masuala ya migogoro ya ndoa.
“Unapozungumzia jamii ni lazima utaje maofisa ustawi wa jamii,kwani jamii leo inamatatizo mengi na watu wa kufuatilia ni maofisa
hao, lakini wamesahaulika nilazima sasa wakumbukwe na wapewe kipaumbele,hali hii itasaidia kuwapa moyo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kupunguza matatizo ya kikatili katika jamii ambayo yanazidi kushika kasi kila kukicha,”alisema.
Bw. Michael alisema fani ya ustawi wa jamii inapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wataalamu wa fani hiyo wanafanya kazi katika mazingira mazuri kwa ufanisi zaidi na kwamba endapo hakutatolewa mkazo katika fani hiyo itafika mahali kutakosekana wataalamu wa ustawi wa jamii hapa nchini.
Akizungumza ofisa ustawi wa jamii sekretarieti ya mkoa wa Kilimanjaro Bw. Sammy Mulemba, alisema pamoja na fani ya ustawi wa jamii kuwa muhimu sana bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo fani hiyo kutopewa kipaumbele kama inavyostahili.
Alisema bado serikali haijaweka mkazo wa kutosha katika fani ya ustawi wa jamii na kuipa umuhimu, hali ambayo inasababisha wataalamu wengi wa fani hiyo kukimbia kazi na kusababisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa wataalamu wa fani hiyo hapa nchini.
Alisema ni vema sasa serikali ikatambua umuhimu wa fani ya ustawi wa jamii na kuwatumia wataalamu wa fani hiyo kushirikiana na jamii kuibua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii na kuzitafutia ufumbuzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment