22 November 2012

'Wakulima epukeni ugonjwa wa batobato


Na Livinus Feruzi
Bukoba.

WAKULIMA wa zao la mhogo katika maeneo ambayo tayari yameathirika na ugonjwa wa Batobato kali, wametakiwa kuepuka matumizi ya mashina ya mihogo yaliyokomaa wakati wa upandaji wa zao hilo ili kuepuka kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo.Wito huo ulitolewa jana na Afisa kilimo kutoka halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoa wa Kagera Bw. Peter Mesashua wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa wakulima wa  mhogo, alizeti na mpunga wa nchi kavu kutoka kata za Kyamulaire, Kyema na Butelankuzi .Mafunzo hayo yanaendeshwa na halmashauri ya wilaya ya Bukoba kwa kushirikiana na asasi za kiraia mkoa wa Kagera (Kangonet ) ni mwendelezo wa kutekeleza mradi wa Kuharakisha kufikiwa kwa malengo ya milenia ifikapo mwaka 2015 kupitia sekta ya kilimo MAF.Alisema katika maeneo ambayo ugonjwa wa Batobato kali ni sugu wakulima hawatakiwi kutumia sehemu ya shina iliyokomaa kupata vipando (miche), kwani sehemu hizo huwa na virusi vingi vinavyosababisha ugonjwa huo kulinganisha na sehemu ambazo zinakuwa bado hazijakomaa.“Kwa miche iliyoathirika sehemu zinazoshauriwa kutumika kwa ajili ya mbegu ni zile sehemu za kati na juu lakini kabla ya kutumika zinatakiwa zipandwe  kwanza kwenye vitalu na baadae ndio zihamishiwe shambani” aliongeza Afisa huyo wa kilimo.Bw. Mesashua aliwataka wakulima kung’oa miche inayobainika kuwa na ugonjwa huo wa batobato na kisha kuichoma, huku akitahadharisha kuwa kuong’oa miche hiyo na kuachwa bila kuchomwa kama inavyofanywa na baadhi ya wakulima ni kuendelea kusambaza zaidi ugonjwa huo.Aidha alionya tabia ya iliyojengeka miongomi mwa wakulima wa zao hilo ya kupeana mbegu na kuzipanda kiholela, kutotembelea mashamba yao baada ya kupanda mazao na kuongeza kuwa hali hiyo inachangia kuendelea kuenea kwa batobato kali ikiwa ni pamoja na mavuno madogo.Bw. Mesashua aliwataka maafisa ugani katika halmashauri hiyo kutekeleza wajibu wao wa kuhakikisha wanasaidia wakulima kupata soko la kuuza mazao yao kwa bei nzuri ili kuondoa tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuwarubuni wakulima na kisha kununua mazao yao kwa bei ya chini.Aliongeza kuwa wakulima wanaweza kuongeza pato lao na kujikwamua kiuchumi iwapo maafisa ugani watatekeleza wajibu wao wa kuwatafutia soko na kuacha kuibiwa na wafanyabiashara, kwani wakulima sio rahisi kufahamu soko ilivyo.Baadhi ya wakulima walisema licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo bado wamekuwa wakiuza mazao yao kwa bei ya chini kutokana na kukosa soko.Mafunzo hayo ya kilimo kupitia mradi wa Maf unafadhiliwa na shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).


No comments:

Post a Comment