22 November 2012

Jiji latakiwa kujenga miundombinu

Na Benedict Kaguo,Tanga


MBUNGE wa zamani wa Viti Maalum CUF Bi Nuru Awadh Bafadhili ameutaka uongozi wa jiji la Tanga kujenga miundombini ya maji taka ili kuwawezesha wananchi kupata mahali pa kumwagia maji taka tofauti na ilivyo sasa.Mbunge huyo alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanawake wa mtaa wa Kombezi A  Kata ya Makorora wakilalamikia kunyanyaswa na kiongozi mmoja wa Idara ya Afya ambaye alilazimika kuwapa adhabu ya kulima na kusafisha mitaro kwa kile alichodai wamekuwa wakitirisha maji machafu barabarani.


Bi Bafadhili alisema Chama cha CUF hakiwezi kuvumilia vitendo vya unyanyasaji wa raia na kutaka hatua za haraka zichukuliwe na Jiji kuboresha mifumo ya maji taka ili kuwawezesha wananchi kupata sehemu ya kumwaga maji hayo machafu.


Alisema sio wananchi wote wenye uwezo wa kuchimba mashimo makubwa ya kuhifadhia maji taka hivyo ni wajibu wa halmshauri ya jiji kuhakikisha inaongeza wigo wa kujenga miundombinu hiyo kwa lengo la kuwaondolea adha wananchi.


Hata hivyo alisema jukumu la maafisa Afya ni kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira na sio kutolea lugha chafu na vitisho  pindi wanapokwenda kusimamia zoezi la usafi la msaragambo ambalo hufanyika kila jumamosi ya kwanza ya kila mwezi.


Wanawake  wa mtaa huo kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kudhalilishwa na baadhi ya watumishi wa afya ambao wamekuwa wakiwatolea lugha chafu na kuwapa adhabu za kulima na kusafisha mitaro pindi wanapokuta maji ya kufulia wamemwaga barabarani kutokana na kutokuwepo kwa mifumo ya maji taka.

No comments:

Post a Comment