21 November 2012

Vodacom yakabidhi bil. 8/- kwa JK


Na Rose Itono

RAIS Jakaya Kikwete, jana amepokea hundi ya sh. bilioni nane kutoka Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania na kuikabidhi katika Hospitali ya CCBRT, ili kufanikisha ujenzi wa Hospitali mpya ya huduma za uzazi na watoto.


Akipokea hundi hiyo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Bw. Rene Meza, Rais Kikwete alisema hayo ni
matokeo ya kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa Fistula
kwa wanawake ambayo ilizinduliwa Februari 18
mwaka huu.

Alisema kutokana na Serikali kujali afya za wanawake na watoto, iliamua kushirikiana na kampuni ya Vodacom Tanzania kuhakikisha ugonjwa huo kwa wanawake unatokomezwa nchini.

Kwa upande wake, Bw. Meza alisema mchango waliotoa ni sehemu ya ahadi zilizotolewa na kampuni hiyo nchini kupitia taasisi yake ya Vodacom Foundation.

“Kati ya fedha hizo, milioni 900 zimetokana na michango ya wafanyakazi wa kampuni hii, washirika pamoja na wadau mbalimbali ambao waliguswa na tatizo hilo.

“Pesa hizi ni nusu ya ahadi yetu kwani awali tuliahidi kuchangia sh. bilioni 15 kwenye ujenzi wa hospitali hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2014,” alisema Bw. Meza.

Alisema kampuni hiyo kupitia taasisi yake ya Vodacom Foundation, CCBRT pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, waliungana pamoja ili kupambana na magonjwa mbalimbali ya uzazi kwa wanawake ukiwemo Fistula ambao umekuwa tishio.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa hospitali hiyo, Bw. Erwin Telemans, aliishukuru kampuni hiyo kwa kutoa fedha hizo na kuahidi kuwa, CCBRT itaendelea kutoa ushirikiano ili kuutokomeza ugonjwa huo.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo ukikamilika, itapewa jina la 'Baobab' na itakuwa ya fufaa kwa wanawake wajawazito ambao
wana matatizo mbalimbali.

Aliongeza kuwa, wanawake milioni mbili duniani wana tatizo la ugonjwa wa Fistula wakati Tanzania ikiwa na wanawake 31,000 wenye tatizo hilo.

Bw. Telemans alisema huduma ya M-Pesa inayotolewa na kampuni hiyo imewezesha wanawake 1,000 wenye matatizo ya Fistula kupata fedha za usafiri na matibabu kutoka mikoani ili waweze kutibiwa katika hospitali hiyo.

Alisema mpango wa kusafirisha wagonjwa kwa kuwatumia fedha kupitia huduma ya M-Pesa, umeiwezesha hospitali hiyo kupambana na ugonjwahuo kwa kuwafikia wanawake wengi hasa waishio vijijini.

“Tunao mabalozi wetu katika mikoa mbalimbali nchini, wanapopata taarifa kuhusu mwanamke mwenye Fistula wanatupa taarifa na pesa inatumwa kupitia M-Pesa na wagonjwa wanapofika Dar es salaam hupokelewa na kuletwa katika hospitali hii,” alisema.

No comments:

Post a Comment