23 November 2012

Tanzania kupeleka Wanajeshi DRC *Membe ahuzunishwa na msimamo wa UNNa Darlin Said

TANZANIA ipo tayari kupeleka wanajeshi 1,000 nchini Congo (DRC), wakaungane na wanajeshi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jeshi la nchi za
Maziwa Makuu ili wakapambane na waasi wa Kundi cha
M23 ambacho kimeuteka mji wa Goma.

Waziri wa Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutumia fursa hiyo kulaani hatua ya waasi hao kuteka mji huo uliopo DRC na kutishia kusonga mbele.

Alisema Tanzania inasikitishwa na kitendo cha Umoja wa Mataifa (UN), kutochukua hatua za haraka ili kuwadhibiti waasi hao badala yake umekuwa ukiyazuia majeshi ya SADC na Maziwa Makuu yasipeleke wanajeshi wake DRC kudhibiti hali hiyo.

“UN inadai wao wana wanajeshi 15,000 ambao wanaweza kupambana na waasi hao, tatizo lililopo majeshi ya Umoja
wa Mataifa yanafanya kazi chini ya kifungu namba sita.

“Kifungu hiki kinawapa fursa ya kulinda amani tu si kupigana,
hali hiyo inachangia waasi hao wazidi kuwa na kiburi cha
kuendeza mapambano dhidi ya Serikali ya DRC,” alisema.

Aliongeza kuwa, umefika wakati wa UN kuangalia namna ya kutumia kipengele namba saba kinachoruhusu majeshi yake,
yale ya SADC na nchi za Maziwa Makuu kuwasambaratisha
waasi hao.

“Hadi sasa UN inatumia kipengele namba sita ambacho hakiruhusu wanajeshi wake kupambana na waasi, kipengele hicho kinawataka wanajeshi hao kuangalia amani, hali inavyoendelea na kutoa
huduma za kiusalama na si kupigana,” alisema Bw. Membe.

Alisema nchi za Maziwa Makuu na SADC, walijitahidi kukaa mezani na UN ili kuishawishi iridhie matumizi ya kipengele
namba saba lakini ilikataa wakidai jeshi lao lipo.

Bw. Membe alisema kutokana na hali hiyo, hali nchini DRC imeendelea kuwa mbaya na kusababisha waasi hao kuuteka
mji wa Goma.

Alitoa wito kwa kikundi hicho kuacha mapigano mara moja kwani mazungumzo ya kutafuta suluhusho la kudumu bado yalikuwa yakiendelea na kama mapigano hayo yataendelea kushika kazi
Tanzania ndio itakayoathirika kwa kuhifadhi wakimbizi.

“Machafuko haya yakiendelea Tanzania ndio itakayoathirika kwa kupokea wimbi la wakimbizi hivyo ni lazima Kikundi cha M23 kiache mapigano mara moja.

“UN isikubali kuona watu wanakufa na kudhalilishwa kwa kuwa walituambia tusiende basi wasikwepe majukumu yao ya kulinda amani,” alisema Bw. Membe.      

Wakati huo huo, Bw. Membe alisema kutokana na hali hiyo, SADC na nchi za Maziwa Mkuu leo zitakutana mjini Kampala nchini Uganda na Serikali ya DRC pamoja na ile ya Rwanda ili kutafuta suluhisho la kudumu.

Alisema katika kikao hilo, wanatarajiwa kutoa maamuzi magumu kama UN itaendelea na msimamo wake wa kukataza majeshi yao yasipambane na waasi waliovamia mji wa Goma.

No comments:

Post a Comment