19 November 2012

Mwandishi Aidan Libenanga afariki



Na Mwandishi Wetu, Morogoro

MWANDISHI wa habari mwandamizi aliyewahi kufanya kazi katika vyombo mbalimbali nchini likiwemo shirika la habari
nchini (SHIHATA), Aidan Libenanga (pichani), amefariki dunia jana, mkoani Morogoro kwa shinikizo la damu.

Akizungumza na gazeti hili, Bw. Ramadhani Libenanga ambaye ni mtoto wa marehemu na mwandishi wa gazeti hili mkoani Morogoro, alisema baba yake alifariki dunia baada ya kufikishwa Hospitali ya Mkoa huo saa 1.00 asubuhi.

Alisema Mzee Libenanga aliamka nyumbani kwake Mtaa wa Sabasaba, saa 11.30 alfajiri ili afue nguo zake lakini na baada
ya kuingia bafuni alidodoka na kukimbizwa hospitali.

“Mzee Libenanga huwa anapenda kufua nguo zake mwenyewe hivyo aliamka asubuhi ili afue lakini alipoingia bafuni ghafla alidondoka hivyo tulimkimbiza Hospitali ya Mkoa kwa
matibabu,” alisema Bw. Libenanga.

Marehemu Mzee Libenanga alizaliwa Kijiji cha Libenanga, Tarafa ya Mwaya, Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Mwaya na sekondari katika shule ya wavulana ya Kwiro, iliyopo Mahenge wilayani humo.

Alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Mzumbe kwa masomo ya kidato cha tano na sita na hatimaye kuajiliwa kama mtumishi wa Shirika la Posta na simu nchini.

Mwaka 1975, mzee Libenanga alikuwa miongoni mwa waandishi wachache waliochaguliwa na Serikali kwenda kusomea taaluma ya Uandishi wa Habari nchini Yugoslavia na kupata cheti cha astashahada na stashahada ya uandishi.

Ameacha mjane, watoto 10 na wajukuu 10, Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu, Aidan Libenanga, Amina.

No comments:

Post a Comment