26 November 2012

Makene Juma Chipukizi wa Hoilers mwenye ndoto za kucheza NBA


Na Victor Mkumbo

KATIKA sanaa mbalimbali ikiwa ni pamoja michezo ya aina tofauti, kumekuwa na vipaji lukuki ambavyo vinajitokeza kila siku.


Hata hivyo wachezaji wengi pamoja na wasanii nchini, wamekua wakifikia malengo kutokana na kujikuta wanapenda fani hizo kwa kuvutiwa na mtu ambaye anafanya vizuri zaidi katika nyanja mbalimbali.

Makene Juma ni mmoja wa wachezaji wa mchezo wa mpira wa Kikapu ambaye ameibukia katika mchezo huo tangu akiwa anasoma katika Shule ya Sekondari ya Hananasif ya Dar es Salaam.

Mchezaji huyo ameanza kuona matunda ya kuupenda mpira wa Kikapu baada ya kupata namba na kuanza kuichezea Klabu ya Hoilers ambayo ipo katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Taifa na inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

"Nilianza kucheza mpira kikapu nikiwa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Hananasifu  baada ya kufikiri kwa makini na kuamini kuwa nitaweza kufanikiwa kuliko kuendelea kucheza soka."


Mchezaji huyo anasema baada ya kuhitimu kidato cha nne mwaka jana na kujinga na kikosi cha timu B amefanikiwa kupandisha kiwango baada ya kupata maelekezo kutoka kwa kocha wake.

"Nimepata uzoefu wa kutosha baada ya kujiunga na Hoilers na ninaamini ikiwa nitazingatia mazoezi nitafanikiwa kucheza nje ya nchi katika ligi ya NBA nchini marekani ambayo ndiyo ndoto yangu kubwa," anasema Juma.

Nyota huyo anaechipukia katika mchezo wa mpira wa kikapu anasema changamoto anazokutana nazo ni uchache wa viwanja vya kufanyia mazoezi kitu ambacho kinasababisha kurudisha nyuma ndoto kufika mbali kupitia mchezo huo.

Hivyo anaiomba Wizara husika kufanya kazi ya ziada kujenga viwanja vingi vya mchezo huo ili kutoa fursa kwa vijana wengi kujifunza mchezo huo na kuwaepusha kujiunga na makundi hatarishi.

Anasema tangu mchezaji wa mpira wa kikapu Mtanzania, Hashimu Thabiti anaecheza ligi ya NBA nchini Marekani alipokuja nchini kuzindua mkakati wa kuendeleza vijana kushiriki mchezo huo, wengi wamehamasika .

"Idadi ya vijana kupenda na kucheza kikapu imeongezeka baada ya Thabiti alipokuja kutoa hamasha katika mchezo huu ila kinachokatisha tamaa ni upungufu wa viwanja vya kuchezea, anasema Juma."

Mchezaji huyo anaemudu kucheza namba tatu anasema mchezaji anaemuhusudu ni Alfa Kisusi ambaye kwa sasa yuko Canada akicheza katika Memorial nchini humo.

Anasema alimuona kwa mara ya kwanza wakati akiwa hapa nchini akicheza timu ya Savio na kutokana na umahiri wake akafanikiwa kupata na timu nchini Canada.

Juma anasema kuwa changamoto nyingine ambayo anakumbana nayo ni uchache wa vifaa vya kufanyai mazoezi ambayo pia inawakabili wachezaji wengi wa mpira wa kikapu.

Mchezaji huyo aliyezaliwa Oktoba 1992 jijini Dar es Salaam anasema ni vyema Makampuni yajitokeze kwa wingi kusaidia ufadhili wa vifaa kwa wachezaji wa mchezo huo kitu ambacho kitawavuta vijana wengi.

"Mtaani kuna vijana wengi ambao hawana kazi za kufanya hivyo ni wakati muhafaka kwa taasisi mbalimbali kujitokeza kusaidia vifaa ambavyo itakuwa chachu kwa vijana wasiokuwa na fedha ya kununulia vifaa kuendelea kushiriki katika mchezo wa mpira wa Kikapu" anasema.

Juma anasema kutokana na umahiri wake wa kucheza mchezo huo wakati akiwa shuleni ambako alitoa mchango mkubwa wa kufanya vyema katika mashindano mbalimbali juhudi binafsi ndio zimemfanya afike mahali alipo kwa sasa.

Hivyo anasema kuwepo katika kikosi cha shule hiyo pia kunamuongezea maarifa zaidi ya kufanikisha ndoto yake ya kufika kimataifa kutokana na wakati wote kuwa katika hali ya mashindano.

Anasema kwa sasa anajivunia kupata namba ya kudumu katika kikosi cha timu yake ya sasa baada ya kufanya jitihada kubwa katika mazoezi ambayo matunda yake yamaenza kuonekana.

Juma, anawaomba vijana wasioshiriki katika michezo kujitokeza kujiunga katika mchezo huo ili kuondokana na tabia hatarishi zinazoweza kuwaharibia maisha yao.

Anaweka wazi kuwa ikiwa vijana watajitokeza katika michezo nchi itanufaika kwa kuwa na wachezaji wengi ambao kwa njia moja au nyingine wataweza kulisaidia taifa na kupata wachezaji wazuri.

"Nawashauri vijana ambao wanaona wana uwezo, kujiunga na timu mbalimbali ili kuweza kufikia malengo yao" anasema.

No comments:

Post a Comment