23 November 2012

'Katiba Mpya ivibane vyama vinavyoshika dola'


Na Mwandishi Wetu, Mara

MKAZI wa Kata ya Mliiba, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Bw. Marco Magubo (31), amependekeza kuwa Katiba Mpya ikataze vyama vya siasa vinavyoingia madarakani baada ya kushinda Uchaguzi wa Rais, visipeperushe bendera ya chama badala
yake vitumie bendera ya Taifa.


Bw. Magubo aliyasema hayo jana wakati akitoa maoni yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mjini humo na kuongeza kuwa, kitendo cha kupeperusha bendera ya chama ambacho kimeingia madarakani kitaongeza chuki kwa wanachama wa vyama
vingine vilivyoshindwa katika uchaguzi huo.

Alisema Rais anayeingia madarakani madarakani anawakilisha masilahi ya Watanzania wote hivyo si busara kwa chama husika kilichoshinda katika Uchaguzi Mkuu kupeperusha bendera ya
chama chao kwani Rais haongozi wanachama wa chama chake pekee bali wananchi wote.

“Tazama nchini Marekani ambao hivi karibuni walifanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, katika kampeni za vyama vyao hatukuona bendera za Chama cha Republican au Democracy ambavyo vyote vilishiriki uchaguzi badala yake tuliona wananchi wakipeperusha bendera ya Taifa lao pekee,” alisema Bw. Magubo.

Aliongeza kuwa, Tanzania ni nchi ya umoja, amani na mshikamano hivyo ni vyema Katiba Mpya iweke kipengele cha kukataza bendera za vyama vya siasa kwani kiongozi ambaye atachaguliwa ana dhamana ya kuwahudumia wananchi wote.

Mshiriki mwingine wa mkutano huo Bw. Lucas Marwa (60), alisema Katiba Mpya ipunguze idadi ya vyama vya siasa na kufikia sita kwani vikiwa vingi ndio mwanzo wa vurugu wakati wa uchaguzi.

Alisema idadi ya vyama vilivyopo kwa sasa nchini havina masilahi kwa wananchi badala yake vimekuwa vikiwachanganya wananchi wakati wa uchaguzi.

“Kwa mfano, hivi sasa Tanzania ina vyama 26 vya siasana ambavyo vyote vikishiriki uchaguzi wakati wa kampeni vimekuwa vikipita kwa wananchi kuomba ridhaa ya kuingia madarakani, binafsi naomba vipunguzwe,” alisema.

Aliongeza kuwa, kama Katiba Mpya itapunguza idadi ya vyama hivyo itawasaidia wananchi kupata viongozi wazuri hasa katika nafasi ya ubunge na udiwani ambayo huwa na wagombea zaidi ya 20 kutoka vyama mbalimbali.

Bw. Marwa alisema wakati wa uchaguzi kumekuwa kukiibuka vyama tofauti na kwenda kufanya kampeni ya kuomba ridhaa ya kushika uongozi lakini vyama hivyo tangu awali vimeshindwa
kuwa na tawi katika eneo husika.

Alisema wagombea wa vyama hivyo wanapokwenda kufanya kampeni za uchaguzi wamekuwa wakiwachanganya wanananchi ili waweze kumpata kiongozi bora.

No comments:

Post a Comment