23 November 2012

Dk. Slaa: CCM itekeleza sera ya elimu bure kwa vitendo



Na Livinus Feruzi, Karagwe

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema hakina tatizo na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutekeleza sera yao ya elimu bure na kushushwa kwa gharama ya vifaa vya ujenzi ili kuchochea maendeleo ya Watanzania.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Willibrod Slaa, aliyasema hayo jana Mjini Karagwe, mkoani Kagera wakati akifungua kikao cha Baraza la chama hicho la Mashauriano la Mkoa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa majimbo yote mkoani humo, Wenyeviti wa CHADEMA na Makatibu wao kutoka mikoa yote nchini na kuongeza kuwa, mwaka 2010 chama hicho kilinadi sera zake kwa Watanzania ikiwemo ya elimu bure.

Sera nyingine ni ile ya kushusha gharama ya vifaa vya ujenzi ili Watanzania wengi wapate fursa ya kujenga nyumba bora kwa ajili ya makazi lakini CCM ilidai sera hizo haziwezi kutekelezeka.

Dkt. Slaa alidai kuwa, CCM pamoja na kudai chama chake hakina uwezo wa kutekeleza sera hiyo lakini baada ya kufanya Mkutano wao Mkuu mjini Dodoma hivi karibuni, chama hicho kilifikia uamuzi wa kuishauri Serikali itoe elimu bure pamoja na
kushusha gharama za vifaa vya ujenzi.

Alisema kutokana na hali hiyo, CHADEMA hakina wivu wa
kuona sera zake zinaanza kutekelezwa na CCM kwani itasaidia kuwaletea manufaa Watanzania.

Dkt. Slaa alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, hivi sasa
chama chao ndio kinaongoza nchi ambapo CCM inatawala
na kuhadharisha kuwa, kama watashindwa kutekeleza sera
hizo wataondoka madarakani 2015.

“Sisi hatuna wivu kama CCM watachukua sera zetu na kuzitekeleza lakini wakishindwa hii ndio itakuwa njia ya kuwaondoa madarakani mwaka 2015,” alisema Dkt. Slaa.

Akiongeza kuwa, chama chake ndio kilichofanikisha kututwa
kwa kodi alizoziita za manyanyaso katika Wilaya ya Karatu na
kusisitiza CCM walitumia sera hiyo na kuondoa kodi za
namna hiyo karibu maeneo yote nchini.

Alisema CHADEMA pia walianzisha sera ya kujenga zahanati katika kila kata iliyoanzia wilayani Karatu na kudai kuwa CCM
baadaye walitangaza kuanzisha utaratibu wa kujenga zahanati
kila kata nchi nzima.

No comments:

Post a Comment