23 November 2012

Mbunge awashawishi wananchi kuwacharaza viboko watendaji


Na Sophia Fundi, Karatu

Mbunge wa Karatu, mkoani Arusha, Mchungaji Israel Natse (CHADEMA), amewataka wananchi kuwacharaza viboko
watendaji wote wanaokaa ofisini badala ya kwenda kwa
wananchi kusikiliza matatizo yanayowakabili.


Alisema wapo baadhi ya watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakikaa ofisini badala ya kwenda kwa wananchi hivyo kukwamisha maendeleo na kuwataka waache tabia hiyo mara moja

Mchungaji Natse aliyasema hayo mjini Karatu juzi wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Qangded, katika ufunfuzi
wa nyumba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Murus ambayo ujenzi wake umegharimu sh. miloni 27.6, kwa nguvu za wananchi na Serikali.

Alisema maendeleo ya kijiji hicho yataletwa na wananchi wenyewe hivyo aliwataka kuwa na moyo wa kuchangia maendeleo ya kijiji chao badala ya kusubiri wafadhili wa ndani na nje ya nchi.

Shule hiyo inakabiliwa na tatizo la upungufu wa mashimo ya vyoo 14 vya wanafunzi ambayo ujenzi wake utagharimu sh. milioni sita ambapo Mchungaji Natse alichangia sh. milioni nne.

Akizungumzia changamoto hizo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Moshi Darabe, alisema shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa waalimu kwani hadi sasa ina mwalimu moja anayefundisha darasa
la kwanza hadi darasa la nne pamoja na Mwalimu Mkuu.

Aliiomba Serikali kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho kulipatia ufumbuzi tatizo la uhaba wa walimu kwani hivi sasa wananchi ndio waliobeba jukumu la kuajiri walimu wakati kipato chao ni kidogo.

Bw. Darabe alisema walifikia uamuzi wa kujenga shule hiyo baada ya wanafunzi kutembea kilometa zaidi ya nene hadi ilipo shule ya Mama ya Qangded ambapo wakati wa msimu wa mvua wanafunzi hawaendi shule kutokana na korongo kubwa wanalopaswa kulivuka.

Akizungumzia changamoto hizo, Mkurugenzi wa Halamshauri ya
Wilaya hiyo, Clement Berege, alikiri shule hiyo kukabiliwa na tatizo la uhaba wa waalimu na kudai kuwa, ifikapo Januari 2013 tatizo hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment