23 November 2012

Alichosema Rais Mbeki ni muhimu kuzingatiwa kwa masilahi ya nchi



RAIS mstaafu wa Afrika Kusini, jana alikutana na viongozi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara kujadili changamoto
mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika.


Kikao hicho kilifanyika jijini Dar es Salaam ambapo ambapo
pamoja na mambo mengine, Rais Mbeki alisema Tanzania imeshindwa kupiga hatua ya maendeleo kwa sababu ya
viongozi wenye umri mkubwa kung'ang'ani madaraka.

Aliongeza kuwa, pamoja na mipango mizuri ya maendeleo
iliyopo nchini tatizo kubwa lililopo ni utekelezwaji wake
ambapo hali hiyo inachangiwa na baadhi ya viongozi
kuendelea kung'ang'ania madaraka.

Alisema viongozi wa Tanzania wanapaswa kutekeleza mipango waliyonayo kama ilivyo katika nchi nyingine ili Taifa liweze kuondokana na umaskini uliopo na kufikia malengo yaliyopo.

Rais Mbeki alisema Tanzania ina mipango mizuri katika
sekta ya kilimo lakini utekelezwaji wake ndio tatizo.

Sisi tunaungana na Rais Mbeki juu ya kauli yake kuwa upo umuhimu wa Serikali iliyopo madarakani kutekeleza mipango
yake ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa ili kuchochea
maendeleo ya sekta mbalimbali.

Wapo baadhi ya wazee katika vyama vya siasa na serikalini ambao wamedumu muda mrefu katika nafasi walizonazo hivyo kukosa maarifa mapya ya kubuni miradi ya maendeleo au kutekeleza mikakati inayoweza kuwaondoa Watanzania katika umaskini.

Kutokana na mabdiliko ya tekonolojia upo umuhimu wa kuwa na viongozi vijana katika ngazi mbalimbali ambao watahimili mikiki
ya mipunduzi ya kiuchumi ambayo ndio msingi wa Watanzania kupiga hatua ya maendeleo.

Vijana wana maarifa, nguvu, ari na uzalendo wa kutumikia vyama vyao vya siasa na Taifa kwa ujumla hivyo wanastahili kupewa
nafasi si kwa maana ya kuwaacha wazee la hasha, bali nao
watakuwepo katika nafasi nyingine hasa za ushauri.

Imani yetu ni kwamba, uongozi wa kuachiana madaraka utasaidia kuleta mapinduzi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ili dhana
ya maisha bora kwa Kila Mtanzania iweze kufikiwa.

Umefika wakati wa Tanzania kujipanga na kuweka mfumo mzuri
wa kuteua viongozi wenye nguvu na uwezo wa kutumikia nafasi wanazopewa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Ili kufikia maendeleo yanayotarajiwa na Watanzania wengi, hatua tuliyofikia tunahitaji viongozi makini wenye uzalendo, wanaozijua vizuri sera za nchi, vyama vyao vya siasa pamoja na uwezo wa kuisimamia Serikali na watendaji waliopewa mamlaka.

1 comment:

  1. CHA MAANA NI UWEZO NA TUSICHAGUE KWA UMRI, UKABILA, UDINI, UKANDA ,USHABIKI WA CHAMA NA KUTOJUA TU. MBONA HATA VIONGOZI WA VYAMA WANAOONGOZA NI WAZEE TU PIA.

    ReplyDelete