23 November 2012

DC Korogwe sasa 'atapika nyongo' kwa wanasiasaNa Yusuph Mussa, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, jana 'ametapika nyongo' baada ya kuwapasha wanasiasa wilayani humo kuwa hana mpango wa kugombea ubunge wala Uenyekiti wa halmashauri hiyo na kudai kuwa nafasi aliyonayo ni ya kuteuliwa na Rais ambaye ndiye anayeweze kumuondoa.


Bw. Gambo aliyasema hayo mbele ya Mbunge wa Korogwe Mjini Bw. Yusuph Nassir na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa huo Bw. Angelo Bendera katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo iliyokaa kuchagua wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya.

“Mimi siwezi kugombea ubunge au nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri, nimekuja hapa kama Mkuu wa Wilaya, lakini pia nafasi ya Mkuu wa Wilaya haigombewi, bali ni uteuzi ambao unafanywa na Rais ambaye ndiye anayeweza kunihamisha
au kunipa kazi nyingine,” alisema Bw. Gambo.

Alisema wapo baadhi ya watu ambao wanalalamika kuingiliwa katika nafasi zao na kusema huko si kuingiliwa bali wanachotakiwa
ni kuwajibika kutokana na nafasi walizopewa.

“Kama kuna mtu anataka kugombea nafasi yako hilo ni suala jingine, lakini mimi ninachotaka ni kila mtu atimize wajibu wake, watu hawaichukii CCM, bali sisi wenyewe ndiyo tunatengeneza mazingira hayo...lazima tuambiane wakati wa kutangaza nafasi za kugombea bado,” alisema Bw. Gambo.

Aliwaataka madiwani kuacha urafiki na watendaji wa halmashauri, kwani uzoefu unaonesha kama diwani ana urafiki na mtendaji kazi haziwezi kwenda kwa kuwa diwani ndio msimamizi wa utekelezaji Ilani ya CCM, hivyo atashindwa kumkemea mtendaji mbovu.

Katika mkutano wa afya uliofanyika hivi karibuni mjini KOrogwe, baadhi ya wananchi walisema kama Bw. Gambo, atagombea ubunge mjini humo watampa ubunge kwani amefanya mambo mengi tangu ateuliwe na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.

Kazi moja wapo iliyofanywa na Bw. Gambo ni kununua trekta la kubeba taka ngumu mjini Korogwe.

Kauli hiyo ilijibiwa bungeni na Bw. Nassir wakati akichangia Bajeti ya Ofisi ya Rais (Menejimenti na Utumishi wa Umma) kwa kusema, Bw. Gambo anaingilia kazi zisizo zake, huku akidai Mkuu huyo wa Wilaya anawapigia debe wanaowania ubunge kwenye jimbo lake.

No comments:

Post a Comment