05 October 2012

Rugambwa kuzikwa rasmi kesho



Na Salma Mrisho, Bukoba

MASALIA ya mwili wa aliyekuwa Kardinali wa kwanza Mwafrika Mwadhama Laurian Rugambwa, ambaye awali alizikwa kwenye Kanisa Katoliki la kwanza lililopo Kashozi mwaka 1997, mkoani Kagera, kesho yatazikwa rasmi katika Kanisa Kuu Jimbo Katoliki mjini Bukoba, baada ya ukarabati wake kukamilika.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki mjini Bukoba, Methodius Kilaini,  mazishi hayo yameambatana na kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa kwake.

Alisema Kardinali Rugambwa alizaliwa Julai 12,1912 ambapo mazishi hayo ni kumbukumbu muhimu kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla.

“Huyu ni Kardinali wa kwanza Afrika na Askofu wa kwanza Mwafrika, hivyo tunategemea kupata wageni wengi kutoka
ndani na nje ya nchi.

“Baada ya mazishi yake, kanisa hili litaanza kutumika kwa ibada za kawaida ili  kuwaondolea waamini adha ya kusalia katika holi lakini tunaendelea kuhamasisha waamini wachangie fedha za kumalizia  sehemu ya ujenzi iliyobaki,” alisema Askofu Kilaini.

Akizungumzia historia ya Kardinali Rugambwa, alisema alipewa Upadre mwaka 1943,  Uaskofu 1952, Ukardinali mwaka 1960 ambapo mwaka 1969 akawa Askofu Mkuu Jimbo la Dar es
Salaam hadi alipostaafu mwaka 1992.

Akizungumzia mambo aliyofanya Kardinali Rugambwa alisema alianzisha Kanisa Kuu Jimbo la Bukoba, kuleta Seminari Kuu ya Ntungamo na kujenga Shule ya Sekondari Rugambwa.

Pia alifanikisha ujenzi wa Hospitali ya Mugana, kuanzisha VIKOBA kwenye Parokia, Seminari Ndogo ya Visiga na Seminari Kuu ya Segerea iliyoko Dar es Salaam.

Kardinali Rugambwa alifariki Desemba 1997 ambapo Askofu Kilaini aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo la kihistoria.

Aliongeza kuwa, wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wamealikwa pamoja na mabalozi ambao wanaziwakilisha nchi zao Tanzania ambapo kanisa hilo limeamua kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Rugamwa ili kumuenzi kwa ajili ya kuendeleza harakati za kukuza elimu kama alivyofanya wakati wa uhai wake.

Kardinali Rugambwa alizaliwa Kijiji cha Bukongo, Parokia ya Rutabo, Kata ya Kamachunu, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera akitokea katika familia iliyotukuka ya kitawala.

Alipata elimu ya Sekondari katika Shule ya Seminari Rubya Junior na kujiunga katika Semiri Kuu ya Katigondo, nchini Uganda, ambako alihitimu masomo ya Falsafa na Theolojia, Desemba 12, 1943.

2 comments: