05 October 2012

Mahabusu atoroka na SMG *Alimnyang'anya Polisi mahakamani



Na Queen Lema, Arusha

MAHABUSU mmoja ambaye jina lake halijafahamika mkazi wa Jiji la Arusha, ametoroka chini ya ulinzi mkali wa askari polisi na kutokomea kusikojulikana.

Mahabusu huyo alifanikiwa kutoroka baada ya kumnyang’anya polisi silaha aina ya SMG, wakati akiwalinda mahabusu katika Mahakama Kuu mjini hapa.

Inaelezwa kuwa, mahabusu hao walikuwa wakitolewa katika chumba walichohifadhiwa ili kupandishwa kalandinga na kurudishwa gerezani.

Tukio hilo limetokea jana saa 7:30 mchana na kuzua hofu kubwa mahakamani hapo ambapo watumishi wa mahakama walijifungia vyumbani wakihofia mahabusu huyo kuwafyatulia risasi.

Taarifa zimedai kuwa, mahabusu huyo alikuwa wa kwanza kutoka katika chumba cha mahabusu na baada ya kumkaribia askari huyo ambaye pia hajafahamika jina lake, ghafla alivaa na kumpora silaha inayodaiwa kuwa na risasi 30, kuruka uzio mrefu wa mahakama na kukimbia.

Mashuhuda wa tukio hilo walidai mahabusu huyo wa jinsia ya kiume, alitokomea na silaha hiyo kwenye Mto Sanawari uliopo pembezoni mwa mahakama hiyo, lakini baadae aliitelekeza silaha hiyo na polisi walifanikiwa kuipata.

“Unajua tukio hili limewshtua watu wengi, hawawatumishi wa mahakama walijifungia ndani wakihofia usalama wao hata watu waliokuwa mahakamani kusikiliza kesi za ndugu zao wote walitawanyika, si jambo la kawaida kutokea tukio kama hili.

“Kuna uzembe umefanywa na polisi, haiwezekeni askari aporwe silaha tene SMG akiwa ameishikilia, hii ni hatari sana,” alisema shuhuda huyo.

Baada ya tukio hilo, polisi walianza kuhaha kumsaka mahabusu huyo ambapo wakati wakipita eneo alilokimbilia walifanikiwa kuikuta bunduki hiyo kwenye mawe yaliyopo katik mto huo.

Hata hivyo haikufahamika mara moja mahabusu huyo alikuwa akikabiliwa na makosa gani mahakamani hapo.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabasi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa wanafanya uchunguzi na msako mkali ili kumpata mahabusu hiyo.


1 comment:

  1. jamani tanzania tunakoelekea ni kubaya sasa,ukakamavu wa police/jeshi la police uko wapi sasa ikiwa askari anapokonywa slaa mkononi mwake.Tena ni mahakani ambapo si rahisi askari kuwa mmoja tu,kama ni mipango imepangwa ili mtu a "save" sawa na si vinginevyo.

    ReplyDelete