03 October 2012

Kesi ya utapeli wa mil. 102/- yakwama



Na Rehema Mohamed

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya utapeli na kujipatia zaidi ya sh. milioni 102 kwa njia ya udanganyifu, umedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.


Washtakiwa katika kesi hiyo Bw. Baraka Rajabu na Bw. George Enos, wote ni wakazi wa Dar es Salaam ambao wanakabiliwa na mashtaka 12.

Mbele ya Hakimu Bi. Augustina Mmbando, wakili wa Serikali Bw. Tumaini Kweka alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.

Hakimu Mbando aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 16 mwaka huuu. Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Aprili mosi na Septemba 8 mwaka huu.

Ilidaiwa katika tarehe hizo, washtakiwa walikula njama ya kutenda makosa hayo ambapo walidaiwa kujipatia sh. milioni 5 kutoka kwa Happyphania Chagonja kama malipo ya kujiunga na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kujipatia zaidi ya sh. milioni 22.2 kutoka kwa Bw. Issa Chikundi, zaidi ya sh. milioni 13.4 kwa Bw. Issa Hossein, sh. milioni 3.7 kwa Bw. Daud Mgonja, zaidi ya sh. milioni 2.30 kwa Kaloti Ngoi, sh. milioni 11.4 kwa Bw. Emanuel Chagonja na zaidi ya sh. milioni 1.4 kwa Bw. Dastan Mkwizo.

Nyingine ni sh. milion 2.2 kutoka kwa Judasino Ngerano, sh. milioni 1.4 kwa Bw. Ibrahim Hashim, sh. milioni 10.5 kwa Bw. Musa Hashim na sh. milioni 29.2 kwa Lauliana Joseph.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuchukua fedha hizo kwa watu hao kama malipo ya maombi ya kujiunga na taasisi hizo.

No comments:

Post a Comment