05 October 2012

Juma Nature kuhamasisha Rocky City Marathon



Na Mwali Ibrahim

MSANII mahiri wa Bongo Flava Juma Kassim Ally a.k.a Sir Nature amejipanga kikamilifu kutoa burudani na kuwapagawisha mashabiki na washiriki wa mbio za mwaka huu za Rock City Marathon zitakazofanyika Oktoba 28, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.


Mbio hizo zimedhaminiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Airtel Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottles, Parastatal Pension Fund (PPF), Geita Gold Mine, TANAPA, Sahara Communication, ATCL, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sir Nature alisema yeye na kundi lake wamejipanga kikamilifu kutoa burudani ya nguvu wakati wa mbio za Rock City Marathon.

“Nitatoa burudani safi kwa mashabiki na wanariadha wenyewe watakaoshiriki Rock City Marathon ya 2012 jijini Mwanza. Mashabiki wangu wa jijini Mwanza wategemee burudani nzuri na wajitokeze kwa wingi kushiriki Rock City Marathon zitakazofanyika Oktoba 28, CCM Kirumba jijini Mwanza.

“Kwakuwa michezo ni afya,nategemea wakazi wengi wa Mwanza watatumia muda uliobaki kujisajili ilitujumuike pamoja , ” alisema Nature.

Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo Grace Sanga kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), alisema  maandalizi ya mbio hizo yanaendela vizuri huku akisema mbio za mwaka huu zimeboreshwa zaidi ikilinganishwa na mwaka jana.

“Maandalizi yanaendelea vizuri na natumia nafasi hii kuomba wananchi ambao mpaka sasa kutumia muda uliyobaki kujisajili. Natumia nafasi hii pia kutoa shukrani kwa wadhamini wetu kwa kutuunga mkono," alisema

Grace alitoa wito kwa wanariadha kujitokeza kusajili na kushiriki mbio hizo na kusema kuwa zawadi za Rock City Marathon ya mwaka huu zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa.

“Mshindi katika mbio za kilometa 21 kwa wanaume na wanawake atajinyakulia shilingi milioni 1.2 wakati mshindi wa pili ataondoka sh.900,000 na watatu sh.700,000.

“Wanariadha watakaoshika nafasi ya nne mpaka ya 10 kila mmoja ataondoka na sh.150,000 na wale watakaoshika nafasi ya 11 hadi 25 kila mmoja atapata sh.100,000," alisema

Alitaja mbio nyingine kuwa ni mbio za kilometa tano kwa watu wote, kilometa tatu kwa watu wenye ulemavu, kilometa tatu kwa wazee (miaka 55 na zaidi) na kilometa mbili kwa watoto wenye umri wa miaka saba hadi 10.

Aidha, Bi Sanga aliwaasa wanariadha kujitokeza na kujisajili ili kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa fomu za usajili zinapatikana katika ofisi za uwanja wa Nyamagana Mwanza.

No comments:

Post a Comment